Jul 28, 2023 12:21 UTC
  • Waislamu Uganda wafanya matembezi kuadhimisha Ashura ya Imam Hussein AS

Waislamu wa medhehebu ya Shia na wapenzi wa Imam Hussein AS huko Uganda wamefanya matembezi ya amani mashariki mwa nchi hiyo, kwa mnasaba wa maombolezo ya Ashura ya Bwana huyo wa Mashahidi.

Huku wakiwa wamevalia mavazi meusi, Waislamu hao wamefanya matembezi ya amani huku wakijipiga vifua, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Hussein AS katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waombolezaji hao yalikuwa na ujumbe usemao "Labbaika Yaa Hussein" huku mengine yakiwa na maandishi yasemayo: Matukio chungu ya Muharram.

Washiriki wengine wa marasimu hayo ya Ashura ya Imam Hussein AS nchini Uganda wameonekana wakimuomboleza mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW na masahaba zake waaminifu kwa kusoma kasida za maombolezo na kujipiga vifua.

Leo Ijumaa, inayosadifiana na siku ya kumi ya mwezi wa Muharram 1445 Hijria ni siku ya Ashura ya Imamu Hussein AS.  Aba Abdillah Al-Hussein AS na masahaba zake waaminifu waliuawa shahidi huko Karbala mnamo tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria.

Marasimu ya Tasua eneo la Bauchi nchini Nigeria jana Alkhamisi

Waislamu nchini Nigeria hapo jana walitumia jukwaa la maombolezo ya Tasua kufanya maandamano ya kulaani vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni katika jimbo la Bauchi hapo jana waliungana na kufanya maandamano makubwa ya kulaani kuvunjiwa heshima na kuchomwa moto kwa makusudi nakala za Qur'ani Tukufu katika nchi za Sweden na Denmark.

Tags