Jeshi la Somalia lawaangamiza magaidi 20 wa Al-Shabaab kusini mwa nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101020-jeshi_la_somalia_lawaangamiza_magaidi_20_wa_al_shabaab_kusini_mwa_nchi
Jeshi la Somalia limetangaza kuwa limewaangamiza wanachama wapatao 20 wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab katika mkoa wa Lower Shabelle kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 13, 2023 14:04 UTC
  • Jeshi la Somalia lawaangamiza magaidi 20 wa Al-Shabaab kusini mwa nchi

Jeshi la Somalia limetangaza kuwa limewaangamiza wanachama wapatao 20 wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab katika mkoa wa Lower Shabelle kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, jeshi la Somalia limeshambulia maficho ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab na kuwaua wanachama 18 wa kundi hilo la kigaidi katika operesheni iliyopangwa na kuratibiwa katika maeneo mawili ya Beldal Amin na Beldal Karim katika mkoa wa Lower Shabelle, kusini mwa nchi hiyo.

Katika operesheni hiyo ya kijeshi, jeshi la Somalia limedhibiti pia maeneo yote yaliyokuwa yakikaliwa na magaidi wa al-Shabaab.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, jeshi la Somalia lilitangaza kuuawa magaidi 100 wa Al-Shabaab wakati wa operesheni ya kijeshi katika eneo la Fima kati ya majimbo mawili ya Shabelle ya Kati na Gholghdod katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Katika mwezi huo huo wa Julai, magaidi wengine 60 wa al-Shabaab waliuawa pia katika operesheni iliyotekelezwa na jeshi la Somalia katika eneo la Bay, kusini mwa nchi.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo lina mielekeo ya itikadi kali na mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, limekuwa likijaribu kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007 na limeshafanya operesheni nyingi za kigaidi na kuua idadi kubwa ya wanajeshi na raia wa nchi hiyo.../