Sep 03, 2023 03:27 UTC
  • Shambulizi la kigaidi msikitini laua Waislamu 7 Nigeria

Genge moja la kigaidi limeshambulia Msikiti mmoja wa jimbo la Kaduna la kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuua Waislamu wasiopungua saba.

Hayo yamesemwa na Msemaji wa Polisi katika jimbo la Kaduna, Mansur Haruna ambaye ameeleza kuwa, shambulizi hilo la kigaidi dhidi ya Msikiti mmoja katika kijiji cha Saya eneo la Ikara lililotokea Ijumaa usiku.

Harun ameongeza kuwa, waumini wengine wawili waliojeruhiwa kwenye shambulizi hilo wanaendelea kutibiwa hospitalini katika eneo la Ikara.

Mkazi wa kijiji hicho, Haruna Ismail, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, "Waumini watano waliuawa kwa kupigwa risasi wakiwa wanaswali Msikitini, na wengine wawili waliuawa kwa risasi nje ya msikiti katika kijiji hicho."

Ikumbukwe kuwa, Septemba mwaka jana, genge jingine la kigaidi liliua Waislamu wasiopungua 15 katika Msikiti mmoja wa jimbo la Zamfara la kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Mashambulio ya kigaidi nchini Nigeria yamesababisha maafa na uharibifu mkubwa hasa katika maeneo ya kaskazini-magharibi na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Magaidi hao ambao aghalabu ya wanafungamana na kundi la Boko Haram na Daesh (ISIS) wameshateka nyara maelfu ya watu na kuua mamia, mbali na kuhatarisha usalama wa kusafiri na kwenda mashambani katika maeneo hayo. 

Tags