Magaidi wa Lakurawa waua watu 34 kaskazini mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136824-magaidi_wa_lakurawa_waua_watu_34_kaskazini_mwa_nigeria
Kwa akali watu 34 wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa Lakurawa kwenye vijiji kadhaa katika jimbo la Kebbi, kaskazini magharibi mwa Nigeria, ripoti ya usalama iliyoonekana na Reuters ilisema Alkhamisi.
(last modified 2026-02-20T03:27:16+00:00 )
Feb 20, 2026 03:27 UTC
  • Magaidi wa Lakurawa waua watu 34 kaskazini mwa Nigeria
    Magaidi wa Lakurawa waua watu 34 kaskazini mwa Nigeria

Kwa akali watu 34 wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa Lakurawa kwenye vijiji kadhaa katika jimbo la Kebbi, kaskazini magharibi mwa Nigeria, ripoti ya usalama iliyoonekana na Reuters ilisema Alkhamisi.

Lakurawa, kundi jipya la wanamgambo linaendesha harakati zake hasa katika majimbo ya Kebbi na Sokoto kaskazini magharibi mwa Nigeria, ambapo Marekani ilifanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo wanaohusishwa na ISIS mwezi Desemba.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki kuvamia vijiji vitatu katika eneo la Borgu katika jimbo la Niger, kaskazini mwa Nigeria, na kuua takriban watu 32 na kuwateka nyara wengine kadhaa.

Aidha mapema mwezi huu wa Februari, mashambulizi ya kigaidi ya kutisha yaliua watu wasiopungua 170 magharibi mwa Nigeria. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf aliliita shambulio hilo kuwa "kitendo cha kikatili na cha kinyama," ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na hujuma "isiyokubalika" dhidi ya amani na usalama.

Kadhalika wiki hiyo hiyo, wakazi wa jimbo la Katsina lililoko kaskazini ya Nigeria walisema, watu wasiopungua 21 waliuawa kwa kupigwa risasi na washambuliaji waliowaandama walengwa kutoka nyumba hadi nyumba.

Wimbi hili la mauaji ya kigaidi linafanyika wakati ambapo Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza karibuni kuwa Washington imetuma askari 100 sambamba na kufanya mashambulizi ya kijeshi nchini Nigeria kwa lengo la eti kupambana na magaidi wa kundi la DAESH (ISIS/ISIL) kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.