Sep 17, 2023 02:25 UTC
  • Uvunjaji ahadi mwingine wa Troika ya Ulaya kuhusu mapatano ya JCPOA

Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Umoja wa Ulaya Alhamisi usiku, Josep Burrell, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya alitangaza kuwa nchi tatu za Ulaya, ambazo ni Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, zimemwandikia barua zikitangaza kwamba hazitaondoa vikwazo vya makombora dhidi ya Iran, ambavyo muda wake umepangwa kumalizika tarehe 18 Oktoba 2023.

Akikariri madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na nchi tatu hizo za Ulaya kuwa Iran haitekelezi ahadi zake kwa mujibu wa mapatano ya  JCPOA, Burrell ameunga mkono madai hayo na kuongeza kuwa atalifikisha suala hilo mbele ya Tume ya Pamoja ya JCPOA chini ya Mfumo wa Utatuzi wa Migogoro (DRM). Burrell amesema, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa (Troika) wametangaza kuwa Iran haijatekeleza makubaliano hayo tangu mwaka 2019 na kuwa suala hilo halijapatiwa ufumbuzi kupitia mfumo wa utatuzi wa migogoro wa JCPOA, hivyo wanakusudia kutoondoa vikwazo ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza pia imetoa taarifa ikitangaza kwamba, itashirikiana na Ufaransa na Ujerumani, kwa ajili ya kuhamishia ndani ya nchi hizo vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vinavyomalizika muda wake Oktoba ijayo.

Josep Burrell

Kwa mujibu wa vifungu vya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo lilipitishwa Julai 2015, vikwazo vilivyowekwa na baraza hilo dhidi ya shughuli za makombora ya Iran vitaondolewa tarehe 18 Oktoba 2023. Kwa hivyo, hatua ya Troika ya Ulaya ya kuendeleza vikwazo vya makombora dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa azimio nambari 2231 na inachukuliwa kuwa ni kuendelezwa siasa za nchi za Magharibi za kudumisha mashinikizo dhidi ya Iran kupitia JCPOA.

Marekani, ambayo ilijiondoa yenyewe katika mapatano ya JCPOA mwezi Mei 2018, sasa inadai kuwa ina wasiwasi kuhusu kuondolewa kabisa vikwazo vya silaha vya Iran mwezi Oktoba 2023, inajaribu kutumia kila mbinu kupitia washirika wake wa Ulaya kwa ajili ya kudumisha vikwazo hivyo dhidi ya Iran. Kwa upande mwingine, Kongresi ya Marekani hivi karibuni imepitisha mpango ambao unalenga kuzuia uzalishaji na uuzaji nje makombora na ndege zisizo na rubani za Iran na wakati huo huo kuwawekea vikwazo watu wanaohusika na utengenezaji wa makombora na ndege hizo. Kongresi hiyo imeitaka serikali ya Rais Joe Biden kuiwekea Iran vikwazo vipya na kuchukua hatua nyinginezo za lazima ili kuzuia mauzo ya silaha za Iran hususan ndege zisizo na rubani na makombora, katika masoko ya kimataifa.

Pamoja na hayo, tajriba ya miaka ya hivi karibuni inaonyesha wazi kwamba, hatua hizo hazijafanikiwa popote katika kuzuia ustawi wa teknolojia ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran. Wakati wa utawala wa Donald Trump mwezi Oktoba 2020, Marekani ilifanya jaribio lisilozaa matunda la kuzuia kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, jambo ambalo lilishindwa kabisa, hasa kutokana na upinzani wa Russia na China zikiwa wanachama wa Kundi la 4+1.

Sasa Washington inatumai kwamba itaweza kunufaika na msaada wa nchi za Ulaya kwa lengo la kudumisha vikwazo vya makombora dhidi ya Iran. Katika hali ambayo Troika ya Ulaya kufikia sasa imevunja ahadi chungu nzima ilizotoa kwa Iran kwa lengo la kupunguza vikwazo vya upande mmoja, mara tu baada ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa JCPOA, Troika hiyo hiyo katika kipindi cha utawala wa sasa wa Biden, imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika kushadidisha mashinikizo dhidi ya Iran, na hii inaonyesha wazi kuwa Wazungu wanaendelea na mkondo wao wa kuvunja ahadi wanazotoa kwa upande wa pili.

Mapatano ya JCPOA

Hii ni katika hali ambayo Umoja na Troika ya Ulaya daima zimekuwa zikikataa kutekeleza majukumu yao na kuituhumu Iran, bila kutoa hoja yoyote ya maana, kuwa inakiuka makubaliano ya JCPOA. Hili linafanyika katika hali ambayo hatua za Iran za kupunguza hatua kwa hatua majukumu yake katika makubaliano ya JCPOA zimechukuliwa tu kama jibu la kukabiliana na ukiukaji wa ahadi unaofanywa mara kwa mara na nchi za Magharibi, katika fremu ya JCPOA. Tehran imetahadharisha mara nyingi kuhusu matokeo hasi ya Troika ya Ulaya kukiuka  mapatano ya JCPOA. Seyyed Mehdi Hosseini Matin, balozi mdogo katika ubalozi wa Iran mjini London anasema: Kutotekelezwa vipengee vya  JCPOA litakuwa kosa kubwa. Huku akisisitiza kuwa muundo wa JCPOA unapaswa kudumishwa, amesema upinzani kuhusu kuondolewa vikwazo na kutotekelezwa vipengee vya azimio hilo ni kwa madhara ya pande za Ulaya na kusisitiza kuwa pande hizo zinapaswa kuwajibishwa.

 

Tags