Ripoti: Wakenya 100 wamejiunga na ISIS Libya, Syria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10276-ripoti_wakenya_100_wamejiunga_na_isis_libya_syria
Vyombo vya kiintelijensia nchini Kenya vinakadiria kuwa makumi ya raia wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki wamejiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) na kueleleza wasiwasi wao kuwa kundi hilo linaendelea kupanua wigo wake katika kanda ya Afrika Mashariki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2016 02:56 UTC
  • Ripoti: Wakenya 100 wamejiunga na ISIS Libya, Syria

Vyombo vya kiintelijensia nchini Kenya vinakadiria kuwa makumi ya raia wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki wamejiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) na kueleleza wasiwasi wao kuwa kundi hilo linaendelea kupanua wigo wake katika kanda ya Afrika Mashariki.

Taarifa ya vyombo hivyo vya kijasusi imesema Wakenya wapatao 100 wakiwemo wanaume na wanawake wameenda Libya na Syria kwa ajili ya kujiunga na kundi hilo la wakufurishaji katika kipindi cha hivi karibuni. Habari zaidi zinasema kuwa, kamatakamata za vyombo vya usalama hivi karibuni nchini Kenya, zimefichua kuwa kundi hilo la kigaidi linawashawishi watu na hususan tabaka la vijana kujiunga nalo na kisha kuwatuma katika nchi zingine duniani, jambo ambalo limeibua hofu kuwa huenda katika siku za baadaye watarejea nchini na kutekeleza wimbi la mashambulizi ya kigaidi. Matt Bryden, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la utafiti la Sahan Research lenye makao yake jijini Nairobi amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, Wakenya wanaorubuniwa kujiunga na kundi la Daesh wanasafiri kwenda Libya na Syria kupitia Khartoum, mji mkuu wa Sudan. Mtafiti huyo ameonya kuwa, Kenya iko katika hatari ya kukumbwa na wimbi la mashambulizi yatakayofanywa na raia wake waliopokea mafunzo ya kigaidi nje ya nchi, kama ilivyoshuhudiwa huko Ubelgiji na Ufaransa hivi karibuni. Hii ni katika hali ambayo, nchi hiyo ya Afrika Mashariki inakabiliwa na tishio la kundi jingine la kigaidi la al-Shabaab lenye makao yake katika nchi jirani ya Somalia.