Misri yapinga mpango wa kuindoa Hamas mamlakani Gaza
Serikali ya Misri imeripotiwa kukataa pendekezo la Marekani la kutwaa kwa muda mamlaka katika Ukanda wa Gaza, ikisisitiza kuwa Cairo haitakuwa na nafasi yoyote katika kuondolewa madarakani Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika eneo hilo lililozingirwa.
Hayo yameripotiwa na gazeti la Wall Street Journal ambalo limewanukuu maafisa wa ngazi za juu wa Misri wakieleza kuwa, Rais Abdel-Fattah el-Sisi wa Misri amekataa pendekezo la Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), William Burns la kuitaka Cairo idhibiti usalama wa Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Sisi amesisitiza kuwa Cairo kamwe haitakuwa na nafasi yoyote katika kuindoa madarakani Hamas na kueleza kuwa, nchi yake inataka harakati hiyo ya muqawama isimamie usalama wa mpaka wa Misri na Gaza.
Hivi karibuni pia, Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri alitangaza kuwa Cairo inaliunga mkono taifa la Palestina na msimamo wake huo ni thabiti, na inapinga mpango wa Marekani na Israel wa kuwahamishia Wapalestina kwenye jangwa la Sinai.
Wimbi kubwa la uungaji mkono wa walimwengu kwa wananchi madhlumu wa Palestina hasa wa Ukanda wa Gaza liliongezeka sambamba na kuanza jinai za kinyama za Israel dhidi ya Wapalestina tarehe 7 Oktoba 2023 na hadi leo hii maandamano yanaendelea katika kona mbalimbali za dunia kulaani jinai hizo.
Aidha jana Jumatano, Ayman Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan alipinga mazungumzo ya kujadili kile kilichotajwa kuwa senario tofauti baada ya vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya waliouawa shahidi kutokana na mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo imeongezeka na kufikia 10,569.