Zimbabwe yatangaza 'hali ya dharura' Harare kutokana na kipindupindu
Zimbabwe imetangaza hali ya dharura katika mji mkuu wa nchi hiyo Harare, kutokana na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambo umeua makumi ya watu, mbali na maelfu ya wengine kupata maambukizi.
Meya wa Harare, Ian Makone amesema mripuko wa sasa wa kipindupindu unashabihiana na ule wa mwaka 2008, ambao ulipelekea kutangazwa dharura ya kitaifa baada ya watu 4,000 kupoteza maisha.
Mamlaka za Zimbabwe zimetangaza kuwa, kitovu cha mripuko wa sasa ni eneo la Kuwadzana, viungani mwa Harare, ambapo nusu ya kesi zilizoripotiwa kufikia sasa zimetokea katika eneo hilo.
Kabla ya hapo, serikali ya Harare ilitangaza hatua kadhaa za kuzuia kuenea maambukizi ikiwa ni pamoja na kuzuia safari katika maeneo yaliyoathirika, kupunguza idadi ya watu mazikoni hadi 50 na kuzuia watu kusalimiana kwa kupeana mikono au kugawa chakula katika maeneo ya mikutano, sherehe n.k.
Serikali ya Zimbabwe ikishirikiana na Federesheni ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (IFRC) imetangaza kuchukua hatua za kudhibiti kuenea ugonjwa wa kipindupindu nchini humo ambapo hadi sasa watu 7,000 wamepata maambukizi tangu mwezi Februari mwaka huu.

Hadi sasa maambukizi kadhaa ya ugonjwa wa kipindupindu yameripotiwa katika majimbo yote 10 ya Zimbabwe, huku kukiwa na ongezeko la kutisha zaidi katika majimbo ya kusini-mashariki ya Masvingo na Manicaland.
Federesheni ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imeonya kuwa, maambukizi ya ugonjwa huo yanaenea kwa kasi, na yumkini yakaingia katika nchi jirani. Nchi jirani za Afrika Kusini, Malawi na Msumbiji zimwahi kukumbwa na mripuko wa kipindupindu huko nyuma.