Waziri Mkuu wa zamani wa Burundi ahukumiwa kifungo cha maisha jela
(last modified Sat, 09 Dec 2023 06:00:42 GMT )
Dec 09, 2023 06:00 UTC
  • Waziri Mkuu wa zamani wa Burundi ahukumiwa kifungo cha maisha jela

Mahakama ya Juu ya Burundi imemhukumu waziri mkuu wa zamani Alain-Guillaume Bunyoni kifungo cha maisha jela baada ya kumpata na hatia ya makosa kadhaa.

Kwa mujibu wa duru za Mahakama ya Juu ya Burundi, katika hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo jana Ijumaa, Bunyoni amepatikana na hatia ya mashtaka kadhaa yaliyokuwa yakimkabili ikiwa ni pamoja na kujaribu kupindua serikali, kumiliki utajiri kinyume cha sheria na kuyumbisha uchumi.
 
Jenerali huyo wa zamani wa jeshi aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Burundi mnamo Julai 2020 na kufukuzwa kazi mnamo Septemba 2022.
 
Kuondolewa kwake kulikuja siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya juu ya kile alichokiita njama ya "mapinduzi" dhidi yake.
Rais Evariste Ndayishimiye (kulia) na Alain-Guillaume Bunyoni

Mahakama ya Juu ya Burundi iliendesha kesi hiyo katika gereza alikokuwa akishikiliwa Bunyoni kuitikia ombi la upande wa mashtaka.

 
Katika hukumu yake hiyo, mahakama iliagiza pia mamlaka husika kutaifisha mali za waziri mkuu huyo wa zamani ambazo ni nyumba na majengo manne pamoja na eneo la ardhi na magari 14.
 
Kwa mujibu wa duru za mahakama, washtakiwa wengine watano waliopandishwa kizimbani wakiwemo washitakiwa wenza wakuu wawili, kanali wa polisi na afisa mwandamizi wa intelijensia, wamehukumiwa vifungo vya kuanzia miaka mitatu hadi 15 jela.
 
Duru hiyo imeongeza kuwa, mshtakiwa wa saba ambaye ni dereva ameachiwa huru.
 
Bunyoni mwenye umri wa miaka 51 alikana mashtaka yote wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa. Wakati huo alisema ilipasa aachiliwe huru kwa sababu ya kukosekana ushahidi.
 
Akiwa mshirika wa karibu wa rais wa zamani Pierre Nkurunziza, Bunyoni alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha CNDD-FDD.../