Dec 15, 2023 10:32 UTC
  • Mahakama Senegal 'yaridhia' kiongozi wa upinzani agombee urais

Mahakama Kuu mjini Dakar imeamuru kusajiliwa upya kwa Ousmane Sonko, kiongozi wa upinzani nchini Senegal katika daftari la wapigakura, na hivyo kumruhusu kuwa mgombea urais.

Uamuzi huo wa jana Alkhamisi utamruhusu Sonko aliyeko kizuizini tangu mwishoni mwa mwezi Julai kwa tuhuma za kuwafisidi vijana, kuwa na matumaini ya kushiriki katika uchaguzi wa rais mwakani. 

Hata hivyo El Hadj Diouf, mmoja wa mawakili wa serikali amesema watakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Diouf amesema uamuzi huu ni ushindi wa muda kwa Sonko ambaye ana hadi Disemba 26 kuwasilisha ombi lake la kuwania urais mwaka ujao. 

Ousmane Sonko anatazamiwa kujitosa rasmi katika kinyang'anyiro cha urais mwezi Februari mwaka 2024, kupitia chama cha Patriots of Senegal for Work, Ethics and Fraternity (PASTEF).

Sonko, 49, ambaye katika uchaguzi wa rais wa 2019 aliibuka mshindi wa tatu, anatuhumu Rais Macky Sall wa Senegal, kwamba anafanya njama za kumzuia asishiriki tena kwenye uchaguzi wa rais. 

Rais Macky Sall wa Senegal anayeelekea kumaliza muda wake wa uongozi

Hii ni katika hali ambayo, Rais Sall, aliyechaguliwa mwaka wa 2012 kuongoza Senegal kwa kipindi cha miaka saba na akachaguliwa tena mwaka wa 2019 kwa ajili ya kipindi cha miaka mitano, alitangaza mapema mwezi Julai kwamba hatagombea tena urais.

Mwishoni mwa Julai, Sonko alihukumiwa kufungwa kwa mashtaka mengine, ikiwa ni pamoja na kuitisha uasi, kushiriki katika uhalifu na kuhatarisha usalama wa serikali.

Tags