Dec 25, 2023 10:43 UTC
  • Watu 16 wauawa katika mapigano jimboni Plateau, kaskazini mwa Nigeria

Kwa akali watu 16 wameuawa katika shambulio la wabeba silaha katika jimbo la Plateau, kaskazini ya kati ya Nigeria.

Shirika la habari la Mehr la Iran limenukuu ripoti ya AFP inayosema kuwa, shambulio hilo limetokea katika kijiji cha Mushu, jimbo la Plateau, eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Vyombo vya habari vya Nigeria vimenukuu duru za kijeshi zikithibitisha habari ya kutokea shambulio hilo katika jimbo la Plateau ambalo limekuwa likishuhudia mapigano baina ya wafugaji na wakulima.

Zaidi ya watu 100 waliuawa katika mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika jimbo hilo linalofahamika pia kama Middle Belt mwezi Mei mwaka huu.

Mashambulizi ya kutumia silaha yamekuwa tishio kubwa la usalama katika mikoa ya kaskazini na katikati mwa Nigeria. Mashambulio hayo yamesababisha vifo na utekaji nyara wa watu wengi wasio na hatia katika miezi ya hivi karibuni. 

Mapema mwezi huu, Jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa, limeua zaidi ya magaidi 180 wanaoaminika kuendesha mashambulizi ya kigaidi katika kona mbalimbali za nchi hiyo.

Edward Buba, Msemaji Taifa wa Jeshi la Nigeria, aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja kwamba takriban watu wengine 204 wamekamatwa na mateka 234 wamekombolewa kwenye operesheni za jeshi hilo.

 

Tags