Wahanga wa shambulio la waasi huko Gatumba, Burundi wazikwa
Wananchi wa Burundi jana Jumanne walijawa na majonzi na vilio wakati watu 19 waliouawa katika shambulio la waasi wa RED- Tabara Ijumaa iliyopita huko Gatumba, wilaya ya Mutimbuzi, jimbo la Bujumbura, kwenye mpaka wa Burundi na Kongo walipozikwa.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Umma, Manaibu Mawaziri na Maseneta pamoja na familia za wahanga.
Serikali ya Burundi imesema kuwa shambulio hilo la waasi lililotekelezwa huko Vugizo limesababisha vifo vya raia 19 na polisi mmoja. Msemaji wa serikali ya Burundi, Jerome Niyonzima, alisema mwanzoni mwa wiki hii kuwa shambulio hilo lilitokea Ijumaa usiku katika kijiji cha Vugizo kulichoko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Watoto 12 na wanawake wawili wajawazito ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo.
Waasi wa RED-Tabara waliwahi kudai kuwa wanapigana dhidi ya serikali ya Burundi kutokea katika kambi mbalimbali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 2015.
Shambulio hili ni la pili kufanywa na waasi wa RED-Tabara katika muda wa wiki mbili. Serikali ya Burundi Jumamosi iliyopita ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ambapo ililaani na kulitaja shambulio hilo la waasi kuwa ni hujuma ya kigaidi.