Dec 30, 2023 11:16 UTC
  • Rais wa Burundi ataka mabadharuli wapigwe mawe hadharani

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi ametoa mwito wa kupigwa mawe hadharani watu wanaojihusisha na ushoga na uhusiano wa watu wenye jinsia moja.

Rais Ndayishimiye alitoa mwito huo jana Ijumaa katika hotuba iliyorushwa mubashara kwenye televisheni ya taifa, ambapo aliitaja ndoa baina ya watu wenye jinsia moja kuwa kitendo cha laana na kuchukiza. 

Amesema, "Binafsi, nadhani iwapo kuna watu wa namna hii (mabaradhuli) Burundi tunapasa kuwapeleka uwanjani na kuwapiga mawe, na kitendo hicho (cha kuwapiga mawe mabadharuli hadharani) si dhambi kwa wanaokifanya."

Kadhalika Rais wa Burundi amezijia juu nchi za Magharibi kwa kuziburuza nchi ndogo kuukumbatia ufuska huo kwa vitisho vya kuzikatia misaada iwapo hazitasalimu amri na kusema, "Hatuhitaji misaada yao, wabaki nayo."

Kadhalika Rais Ndayshimiye wa Burundi amewaonya vikali Warundi wanaoishi ughaibuni na waliokumbatia ubaradhuli kwa kuwaambia, "Ambao wameamua kumfuata shetani kwa kujihusisha na ushoga, wasirejee nchini."

Maandamano ya kupinga ubaradhuli

Burundi ilijinaisha ushoga mwaka 2009, na wanaopatikana na hatia ya kujihusisha na ufuska huo wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka miwili jela. 

Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa kidini, kijamii na kisiasa barani Afrika wameendelea kulaani na kukosoa hatua ya majuzi ya Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ya kutoa idhini rasmi kwa mapadri kufanya sherehe na kubariki ndoa za watu wa jinsia moja katika kanisa hilo.

Tags