Kiongozi wa zamani wa upinzani Chad ateuliwa kuwa Waziri Mkuu
Serikali ya mpito ya Chad imemteua Succes Masra, kiongozi wa zamani wa upinzani ambaye alirejea nchini humo hivi karibuni kutoka uhamishoni, kuwa Waziri Mkuu.
Hayo yalitangazwa jana Jumatatu na Mahamat Ahmad Alhabo, Katibu Mkuu mpya wa Ofisi ya Rais wa Chad ambaye ameongeza kuwa, Masra atahudumu kama Waziri Mkuu katika kipindi chote cha mpito hadi nchi hiyo irejee katika utawala wa kiraia.
Masra, rais wa Chama cha Wanamageuzi amekuwa akipinga vikali utawala wa kijeshi ulioingia madarakani zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Mwanasiasa huyo aliwaasa wafuasi wake waunge mkono Katiba mpya iliyopasishwa karibuni. Haya yanajiri siku chache baada ya Tume ya Uchaguzi nchini humo kutangaza kuwa, rasimu ya Katiba mpya ya nchi hiyo iliyopigiwa kura hivi karibuni imepasishwa kwa asilimia 86.
Chad kwa muda sasa imekuwa ikishuhudia maandamano ya kudai mabadiliko ya demokrasia ambapo hadi sasa makumi ya watu wameuawa na vikosi vya usalama vinavyotuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati linalotawaliwa na jeshi limekuwa katika mgogoro tangu kifo cha Aprili 2021 cha Rais Idriss Deby, ambaye alitawala kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu.