Katibu Mkuu wa Arab League alalamikia ziara ya Benjamin Netanyahu barani Afrika
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amesema kuwa, lengo la Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni la kutembelea nchi kadhaa za Afrika ni kujaribu kuitoa Israel katika dimbwi la kutengwa kimataifa.
Shirika la habari la Mehr limemnukuu Ahmed Aboul Gheit akisema jana kuwa, ziara ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni katika nchi nne za Afrika imefanyika kwa lengo moja tu, nalo ni kujaribu kuitoa Israel katika kutengwa kimataifa kutokana na utawala huo kuendeleza vitendo vya dhulma na kibaguzi huko Palestina.
Ahmed Aboul Gheit ameongeza kuwa, Benjamin Netanyahu anafanya njama za kuhalalisha jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesisitiza kuwa: Umoja wa Afrika AU una misimamo yake ya kimsingi nayo ni kulilinda na kuliunga mkono taifa la Palestina katika jamii ya kimataifa, na hata umetoa tamko lililo lazima kutekelezwa na kila mwanachana wa umoja huo kuhusu suala hilo.
Ziara ya hivi sasa ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni barani Afrika ni ziara ya kwanza ya waziri mkuu wa Israel barani humo baada ya ile iliyiowahi kufanywa na Is'haq Rabin, waziri mkuu wa tano wa Israel wakati alipotembela Morocco mwaka 1994.