Misri yaionya Israel kutoudhibiti Ukanda wa Philadelphi kwenye mpaka wa Palestina
(last modified Tue, 23 Jan 2024 05:34:03 GMT )
Jan 23, 2024 05:34 UTC
  • Misri yaionya Israel kutoudhibiti Ukanda wa Philadelphi kwenye mpaka wa Palestina

Misri imeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba jaribio lolote la kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi inayotenganisha eneo la Wapalestina lililozingirwa la Ukanda wa Gaza na Misri, linalojulikana kama Korido ya Philadelphi, litakuwa ni "tishio kubwa" kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili.

Diaa Rashwan, mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Misri, amesema katika taarifa aliyotoa kupitia mitandao ya kijamii kwamba, "inapasa isisitizwe kwa mkazo kwamba hatua yoyote ya Israel katika mwelekeo huu itakuwa ni tishio kubwa kwa uhusiano wa Misri na Israel".

Rashwan amebainisha kuwa, Misri italichukulia jaribio lolote la Israel la kulikalia eneo la Ushoroba wa Philadelphi kuwa ni ukiukaji wa mikataba ya usalama na itifaki iliyotiwa saini kati ya utawala huo wa Kizayuni na Misri.

Ukanda wa Philadelphi ni kipande cha ardhi cha urefu wa kilomita 14 kilichoko kwenye mpaka wa Misri na Palestina.

Diaa Rashwan

Viongozi wa utawala wa Kizayuni wameshatoa kauli kadhaa kuhusiana na kuinyakua korido hiyo. Baadhi ya mawaziri wenye misimamo mikali na ya chuki katika serikali ya mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mpaka inayoongozwa na Benjamin Netanyahu wametoa wito mara kadhaa wa kufanywa mauaji ya kimbari ili kuwaangamiza Wapalestina wote wa Ukanda wa Gaza.

Rashwan amesema mpaka wa magharibi wa Palestina uko salama na kwamba madai ya Israel kwamba silaha zilikuwa zinaingizwa Gaza kimagendo kutokea Misri ni za uongo.

Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Misri ameongeza kuwa madai hayo yanatolewa na Israel "ili kuhalalisha uendelezaji wa kampeni ya kuwaadhibu na wasiohusika" unayotekeleza utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina uliowawekea mzingiro wa huko Ukanda wa Gaza.

Netanyahu amesikika mara kadhaa akitangaza kuwa eneo la ushoroba wa Philadelphi lazima liwe chini ya utawala haramu wa Israel, hatua ambayo ikitekelezwa itatenganisha eneo la Gaza na Misri.

Misri ina hofu kwamba uvamizi wa kijeshi utakaofanywa na utawala wa Kizayuni kwenye mpaka huo unaweza kusukuma idadi kubwa ya Wapalestina kwenye eneo la ardhi yake.../