Jumuiya ya ECOWAS yaiondolea vikwazo Niger
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS imetangaza habari ya kuiondolea Niger vikwazo vya kiuchumi na kifedha.
Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na ECOWAS imesema, uamuzi huo wa kuiondolea vikwazo nchi hiyo ya Afrika Magharibi umechukuliwa kwa misingi ya ubinadamu.
Baada ya kikao cha faragha cha viongozi wa ECOWAS mjini Abuja Nigeria cha kujadili hali ya kisiasa na usalama katika eneo hilo la magharibi mwa Afrika, jumuiya hiyo imetagaza kuiondolea Niger vikwazo, vikiwemo vikwazo vya kuifungia mipaka, kuzuia mali za Benki Kuu na serikali ya nchi hiyo na kusimamisha miamala ya kibiashara na nchi wanachama.
Weledi wa mambo wanasema ECOWAS imechukua hatua hiyo kwa shabaha ya kujaribu kupunguza msuguano baina ya jumuiya hiyo na Niger pamoja nchi nyingine wanachama wake. Hata hivyo Rais wa Kamisheni ya ECOWAS, Omar Touray amesema vikwazo vya kisiasa na vinavyolenga shakhsia maalum wa Niger vitaendelea kutekelezwa.
Disemba 2023, ECOWAS yenye nchi wanachama 15 ilisimamisha rasmi uanachama wa Niger katika umoja huo wa kikanda, miezi kadhaa baada ya kujiri mapinduzi ya kijeshi, hadi utaratibu wa kikatiba utakaporejeshwa nchini humo.
Niger pamoja na Burkina Faso na Mali, zilitangaza mnamo Januari 28 kwamba zimeamua kujitoa katika ECOWAS na kutuma taarifa rasmi kwa jumuiya hiyo siku iliyofuata.
Kifungu cha 91 cha mkataba wa jumuiya hiyo ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika kinaeleza kuwa nchi wanachama zitaendelea kubaki na wajibu wao kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kuarifu kujiondoa kwao. Lakini nchi hizo tatu, ambazo zote kwa sasa zinaongozwa na tawala za kijeshi zilizoingia madarakani kupitia mapinduzi, zimeamua kutosubiri hadi wakati huo.