Mar 19, 2024 02:38 UTC
  • Sameh Shoukry
    Sameh Shoukry

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema Marekani inapasa kuileza wazi Israel kuhusu taathira hasi na matokeo mabaya ya utawala wa Kizayuni kuushambulia kijeshi mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri alisema hayo jana Jumatatu mjini Cairo katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini na kuongeza kuwa, uvamizi wa nchi kavu huko Rafah unaweza kukata mojawapo ya njia pekee za kusambaza chakula na vifaa vya matibabu vinavyohitajika sana katika eneo la Gaza. 

Shoukry ameeleza kuwa: Haitoshi tu kwa (Marekani) kulaani na kutoka vitisho hewa, na kueleza upinzani wake (kwa hatua ya Israel kuishambulia Rafah), bali inapasa iieleza Israel kuhusu madhara ya kutoheshiwa msimamo huo wa kutoshambuliwa Rafah.

Zaidi ya nusu ya wakazi milioni mbili na laki tatu wa Gaza wamekimbilia Rafah kuepuka hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel katika maeneo mengine, na wamefurika kwenye kambi kubwa za mahema na makazi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa karibu na mpaka.

Wakazi wa Rafah wakihangaika kufuatia uvamizi wa Israel

Mwezi uliopita wa Februari, Misri ilitishia kusitisha mkataba wa amani wa Camp David iliosaini na utawala wa Kizayuni wa Israel iwapo wanajeshi wa utawala huo ghasibu watapelekwa katika mji wa mpakani wa Gaza uliofurika watu wa Rafah, na kusema operesheni ya kijeshi katika mji huo inaweza kulazimisha kufungwa kwa njia kuu ya kusambazia misaada katika eneo hilo.

Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu anasisitiza kuwa kutuma wanajeshi huko Rafah ni muhimu ili "kushinda" vita vilivyodumu kwa zaidi ya miezi mitano sasa dhidi ya Harakati ya Muqawama wa Palestina (Hamas).

Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameongeza kuwa, operesheni ya nchi kavu ya jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya Rafah itasababisha janga kubwa la kibinadamu lisiloelezeka na vifo.

Tags