Wahalifu wenye silaha wawateka nyara watu zaidi ya 100 huko Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i109676-wahalifu_wenye_silaha_wawateka_nyara_watu_zaidi_ya_100_huko_nigeria
Wahalifu wenye silaha wamewateka nyara zaidi ya watu 100 katika mashambulizi mawili mapya kaskazini magharibi mwa Nigeria, ikiwa zimepita wiki kadhaa baada ya wanafunzi 250 wa shule kutekwa nyara nchini humo.
(last modified 2024-03-19T11:49:27+00:00 )
Mar 19, 2024 11:49 UTC
  • Wahalifu wenye silaha wawateka nyara watu zaidi ya 100 huko Nigeria

Wahalifu wenye silaha wamewateka nyara zaidi ya watu 100 katika mashambulizi mawili mapya kaskazini magharibi mwa Nigeria, ikiwa zimepita wiki kadhaa baada ya wanafunzi 250 wa shule kutekwa nyara nchini humo.

Watu hawa zaidi ya 100 wanadaiwa kutekwa nyara na magenge ya wahalifu wanaojulikana huko Nigeria kama majambazi kufuatia visa vya utekaji nyara walivyofanya katika eneo la Kajuru jimboni Kaduna siku kadhaa zilizopita.  Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria anakabiliwa na mashinikkizo ya ndani kufuatia visa vikubwa mtawalia vya utekaji nyara nchini humo. 

Wahalifu hao mara kwa mara huwashambulia raia wa kawaida  katika maeneo ya kaskazini magharibi na kaskazini kati mwa Nigeria ambapo huwapora raia vijijini na kutekeleza utekaji nyara mkubwa mkabala wa kupatiwa mlungula. Visa hivi vya kutekwa raia na magenge ya wahalifu vimepelekea watu wasiopungua milioni moja kuhama makazi yao. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa. 

Ibrahim Gajere Mwenyekiti wa serikali za mtaa amesema kuwa usiku wa kuamkia jana watu wenye silaha waliwateka nyara watu 87 katika kituo cha Kajuru. Baada ya kuwateka nyara wahalifu hao walianza kuwatoa raia majumbani mwao na kuwateka nyara. 

Wakati huo huo Uba Sani Gavana wa jimbo la Kaduna amekutana na wawakilishi wa wazazi wa wanaofunzi waliotekwa nyara siku kadhaa zilizopota na kusema anafanya kila awezalo ili kuwakomboa watoto. 

Uba Sani, Gavana wa jimbo la Kaduna 

Ndugu mmoja wa familia amesema kuwa watekaji nyara wametaka kulipwa fedha nyingi ili kuwarejesha wanafunzi hao, lakini wiki iliyopita Rais Tinubu wa Nigeria alisema kuwa ameviagiza vyombo vya usalama kutolipa fedha hizo.