Mar 21, 2024 02:54 UTC
  • Taharuki yatanda Sudan Kusini baada ya watu 15 kuuawa Pibor

Hali ya wasi wasi imetanda nchini Sudan Kusini kufuatia mauaji ya watu 15 yaliyotokea katika eneo la Pibor, mashariki mwa nchi hiyo.

Abraham Kelang, Waziri wa Habari wa Eneo Pana la Pibor aliliambia shirika la habari la Reuters jana Jumatano kuwa, miongoni mwa waliouawa katika shambulizi hilo la wabeba silaha ni Kamishna wa Kaunti ya Boma, eneo la Pibor.

Amesema msafara wa maafisa wa serikali akiwemo kamishna huyo ulizingirwa na kuanza kumiminiwa risasi na kundi la wabeba silaha, walipokuwa wanatoka katika kijiji cha Nyat siku ya Jumanne.

Habari zaidi zinasema kuwa, Naibu Kamanda wa Jeshi katika kaunti ya Boma, maafisa wa ngazi za juu wa serikali na mlinzi wa Kamishna wa Kaunti hiyo waliuawa pia katika hujuma hiyo ya kushtukiza.

Magenge ya vijana wanaobeba silaha Sudan Kusini

Kelang amesema waliotekeleza shambulizi hilo wanashukiwa kuwa vijana mabarobaro kutoka jamii ya Anyuak ambao wanahusishwa na msusuru wa mashambulizi katika maeneo hayo.

Zaidi ya watu 150 wameuawa kuanzia mwishoni mwa Januari mwaka huu 2024 hadi mwishoni mwa Februari katika mashambulizi na makabaliano baina ya makundi hasimu katika maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Sudan.

 

Tags