Rais Museveni amteua mwanawe kuwa Mkuu wa Majeshi ya Uganda
(last modified Fri, 22 Mar 2024 10:56:20 GMT )
Mar 22, 2024 10:56 UTC
  • Rais Museveni amteua mwanawe kuwa Mkuu wa Majeshi ya Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemteua mwanawe wa kiume, Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuwa Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wizara ya Ulinzi ya Uganda imetangaza habari hiyo leo Ijumaa bila kutoa maelezo ya kina. Taarifa ya wizara hiyo imesema Jenerali Kainerugaba amechukua nafasi ya Wilson Mbasu Mbadi, ambaye jana aliondolewa katika wadhifa huo na kuteuliwa kuwa waziri wa ngazi ya chini katika Baraza la Mawaziri la Museveni.

Jenerali Muhoozi Kainerugaba mwenye umri wa miaka 48 amewahi kuwa Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Uganda, lakini aliondolewa kwenye cheo hicho mwaka 2022 na Rais Museveni, baada ya kutishia kuishambulia nchi jirani ya Kenye kupitia jumbe alizotuma kwenye mitandao ya kijamii. 

Ingawaje sheria za Uganda haziwaruhusu maafisa wa jeshi kujihusisha na siasa, lakini Muhoozi amekuwa akijibizana na kurushiana cheche na viongozi wa upinzani, na tayari ameunda kundi la kulobi linalompigia debe la kisiasa.  

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Museveni, rais wa nne barani Afrika aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi, amekuwa akishutumiwa na upinzani na makundi ya kutetea haki za binadamu kuwa anatumia jeshi kuwadhoofisha wapinzani wake kwa kutoa vitisho, vipigo au kuwasweka jela.

Wadadisi wa mambo wanasema huenda kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 79, na aliyeingia madarakani kwa mtutu wa bunduki mwaka 1986, hatagombea urais kwa muhula wa saba katika uchaguzi ujao unaotazamiwa kufanyika mwaka 2026, na kwamba hatua ya kumteua mwanawe kuwa mkuu wa majeshi ni kumuandaa kurithi mikoba yake.