Apr 29, 2024 07:18 UTC
  • Burkina Faso yapiga marufuku BBC na VOA kwa kutangaza uongo

Burkina Faso imevisimamisha vyombo vya habari vingi vya Magharibi na Afrika kutokana na kutangaza ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu (HRW) inayolituhumu jeshi la nchi hiyo kwa mauaji ya kiholela.

Uamuzi huo unafuatia kusimamishwa pia kwa shirika la BBC na Sauti ya Amerika inayofadhiliwa na serikalini ya Marekani kwa kuripoti uchunguzi wa Human Rights Watch ambao ulidai jeshi la Burkina Faso liliwanyonga wanakijiji wapatao 223 mwezi Februari kama sehemu ya kampeni yake dhidi ya raia wanaotuhumiwa kushirikiana na wanamgambo wa kijihadi.

Baraza la mawasiliano la nchi hiyo ya Afrika Magharibi linaloongozwa na jeshi lilisema matangazo ya televisheni ya Ufaransa TV5 Monde yatasitishwa kwa wiki mbili, huku tovuti yake ikizuiwa.

Taarifa zaidi zinasema, tovuti za shirika la utangazaji la Ujerumani Deutsche Welle, magazeti ya Ufaransa Le Monde na Ouest-France, gazeti la Uingereza la The Guardian, na mashirika ya Afrika ya APA na Ecofin pia yamezuiliwa hadi itakapotangazwa tena baadaye.

Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo, Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso

 

Jana serikali ya Burkina Faso ilikanusha vikali na kulaani tuhuma ilizosema hazina msingi zilizotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ambalo limelituhumu jeshi la serikali ya nchi hiyo kuwa lilihusika na mauaji ya mwezi Februari mwaka huu 2024 katika vijiji vya Nodin na Soro kaskazini mwa nchi hiyo.

Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso, Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo ameeleza kuwa mauaji yaliyojiri katika vijiji vya Nodin na Soro yalipelekea kufunguliwa uchunguzi wa kisheria na kwamba wakati wakisubiri kukamilika uchunguzi huo na kubainika ukweli juu wa wahusika, Human Rights Watch kwa mtazamo wake limeamua kutangaza matokeo ya uchunguzi huo.