Iran: Israel ni nembo ya ugaidi ulioratibiwa duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i111760-iran_israel_ni_nembo_ya_ugaidi_ulioratibiwa_duniani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kama nembo kuu ya ugaidi ulioratibiwa duniani.
(last modified 2024-05-14T08:27:33+00:00 )
May 14, 2024 08:27 UTC
  • Iran: Israel ni nembo ya ugaidi ulioratibiwa duniani

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kama nembo kuu ya ugaidi ulioratibiwa duniani.

Wizara hiyo imesema hayo katika taarifa iliyoitoa leo Jumanne kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 76 ya Siku ya Nakba, itakayoadhimishwa kesho Mei 15.

Tarehe 15 Mei, 1948 ni siku ya janga na maafa kwa watu wote wa Palestina ndani na nje ya ardhi hiyo, inayotambuliwa kwa jina la "Siku ya Nakba" ikiwa ndio mwanzo wa uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu uliofanywa na vuguvugu la Kizayuni, na kubaki bila makazi Wapalestina baada ya kuhamishwa katika ardhi za mababa na mababu zao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Siku ya Nakba inaashiria kuanza enzi za mauaji ya kimbari na umgwaji damu, kufurushwa Wapalestina katika ardhi zao, ardhi zao kukaliwa kwa mabavu, sanjari na kunajisiwa na kuvunjiwa heshima ardhi yao tukufu, kwa baraka na uungaji mkono wa madola ya kikoloni yakiongozwa na Marekani. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu inalaani kwa nguvu zote mauaji ya raia zaidi ya 35,000 wasio na hatia aghalabu wakiwa wanawake na watoto, katika vita vya umwagaji damu vinavyoendelezwa na Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Umwagaji damu za Wapalestina Gaza

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesisitiza kuwa, "Utekelezaji wa jinai za kimataifa, ikiwemo jinai ya kivita, mauaji ya kimbari, na jinai dhidi ya binadamu, unakanyaga thamani za msingi za Umoja wa Mataifa, pamoja na kanununi, sheria na miongozo inayotambulika kimataifa.

Imeongeza kuwa: Watenda jinai wa utawala wa Kizayuni wanapaswa kubeba dhima ya jinai zao, na ukiukaji wao wa sheria za kimataifa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemalizia taarifa hiyo kwa kusema: Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono suala la Palestina kupewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa; na kwamba Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa imefungua mlango wa kuungwa mkono zaidi taifa la Palestina, na kutetewa juhudi zao za kukombolewa ardhi yao ya kihistoria.