Apr 29, 2024 11:10 UTC
  • Watu 45 wapoteza maisha baada ya bwawa kuvunja kingo zake Kenya 

Watu wasiopungua 45 wameripotiwa kupoteza maisha baada ya Bwawa la Old Kijabe kuvunja kingo zake nchini Kenya huku mvua kubwa zikiendelea kusababisha mafuruko nchini humo.

Kamanda wa polisi ya Naivasha Stephen Kirui amethibitisha kisa hicho akibainisha kuwa watu wengine kadhaa wamekimbizwa katika hospitali ya Naivasha kwa matibabu.
Kirui amesema bwawa hilo lilipasua kingo zake na kukata usafiri katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru. Amesema shughuli ya utafutaji na uokoaji inaendelea lakini akaonya kuwa idadi ya walioaga dunia huenda ikaongezeka huku msako ukiendelea.
Naye Gavana Susan Kihika wa Kaunti ya Nakuru amesema vikosi vya uokoaji vinachimba matope na vifusi kujaribu kutafuta manusura karibu na mji wa Mai Mahiu.
Kihika amesema ufikiaji mji huo ulio umbali wa maili 20 kaskazini mwa mji mkuu Nairobi, umekuwa mgumu kwani sehemu ya barabara imekatika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha hivi majuzi. Amesema timu za wokozi zinaondoa uchafu zinapojaribu kuwafikia walionusurika na kufukua miili.

Leo Jumatatu Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema watu kadhaa wamepelekwa katika kituo cha afya huko Mai Mahiu kutokana na mafuriko yaliyoathiri kijiji cha Kamuchiri. 
Kenya imesajili mvua kubwa tangu katikati ya mwezi Machi lakini mvua imezidi kunyesha wiki iliyopita, na kusababisha mafuriko makubwa nchini.
Kwa akali watu 103 wanaripotiwa kufariki dunia nchini Kenya kufuatia mafuriko hayo.