May 02, 2024 11:19 UTC
  • Watetezi wa haki za binadamu wakaribisha hati ya kukamatwa kwa François Bozizé

Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekaribisha na kufurahia kutolewa hati ya kukamatwa kwa François Bozizé Rais wa zamani wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Samira Daoud, mkurugenzi wa shirika la kimataifa la Haki za Binadamu Amnesty International kwa Afrika Magharibi na Kati, kumfungulia mashitaka François Bozizé ni hatua kubwa katika mapambano dhidi ya upuuzaji mambo.

Aidha amesema, tangazo hili kwetu ni hatua ya kutia moyo sana katika kazi hii ya haki kwa waathiriwa. Na linatia moyo zaidi, kwa sababu ni hati ya kukamatwa iliyotolewa dhidi ya washukiwa wa ngazi ya juu.

Naye Joseph Bindoumi, kiongozi wa shirika la Haki za Kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, anatoa wito kwa Mahakama Maalumu ya Jinai kufuatilia kesi zote, bila ubaguzi.

Mahakama Maalumu ya Jinai (CPS) inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, imetoa hati ya kukamatwa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu unaodaiwa kufanywa na jeshi wakati wa uongozi wake.

Uhalifu huo inasemekana ulifanywa na walinzi wa rais wa Bozize na vikosi vingine katika gereza la kiraia na katika kituo cha mafunzo ya kijeshi katika mji wa Bossembele.

Majaji wa CPS wamesema, kutokana na ushahidi mkubwa na madhubuti uliopo dhidi ya Bozize kuna uwezekano wa kumbebesha dhima ya kutenda jinai katika nafasi yake kama kiongozi wa ngazi ya juu na kiongozi wa kijeshi.

Bozize mwenye umri wa 77, alitawala Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia Machi 2003 hadi Machi 2013 alipopinduliwa. Alinyakua madaraka pia kupitia mapinduzi ya kijeshi, na anaishi uhamishoni nchini Guinea-Bissau tangu Machi 2023.