May 02, 2024 11:22 UTC
  • Meja Jenerali Fatuma Ahmed ateuliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza jeshi la anga la Kenya

Rais William Ruto wa Kenya amemteua Meja Jenerali Fatuma Ahmed kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga la nchi hiyo na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo katika historia ya Kenya.

Meja Jenerali Fatuma Ahmed ameandika historia nchini Kenya kwa kuteuliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza kitengo cha jeshi la anga katika majeshi ya Ulinzi ya Kenya, KDF.

Uteuzi wake umetangazwa na idara ya ulinzi baada ya kuidhinishwa na Rais William Ruto ambaye pia amemteua Jenerali Charles Kahariri kuwa mkuu wa majeshi.

Jenerali Kahariri alikuwa anashikilia wadhifa huo akiwa Luteni Jenerali baada ya kifo cha Jenerali Francis Omondi Ogolla mwezi Aprili katika ajali ya ndege.

Mnamo 2017 Rais Uhuru Kenyatta alimteua kuwa Brigedia wa kwamza wa kike katika jeshi la Kenya na baada ya uteuzi wake mabadiliko makubwa ya kuwajumuisha kina mama katika uongozi jeshini yameshuhudiwa kama katika kitengo cha mawasiliano ambacho kinaongozwa na Brigedia Ziporra Kioko, kitengo cha sheria kinachoongozwa na Brigedia Yvonne Kerubo na mkurugenzi wa taasisi ya usalama na amani IPSTC Brigedia Joyce Sitienei, na afisa anayesimamia kitengo cha kubuni ramani Brigedia Caroline Mutisya.

Meja Jenerali Fatuma Ahmed, kamanda mpya wa Jeshi la Anga la Kenya

Katika uteuzi wa Alkhamisi hii Rais ammeteua meja jenerali John Omenda ambaye alikuwa mkuu wa jeshi la anga kuwa Luteni Jenerali na kushikilia wadhifa wa naibu mkuu wa majeshi, Meja jenerali Paul Owuor amekabidhiwa wadhifa wa mkuu wa jeshi la majini huku maafisa wengine wakipandhiswa madaraka kutoka Ubregedia na kuwa meja jenerali na kuteuliwa pia kuongoza tasisi mbalimbali.