Kenya na Uganda zaafikiana kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i111848-kenya_na_uganda_zaafikiana_kuhusu_ujenzi_wa_bomba_la_mafuta
Kenya na Uganda zimekubaliana kujenga kwa pamoja bomba la kusafirishia mafuta kutoka mjini Eldoret katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya hadi Uganda.
(last modified 2024-05-17T07:24:59+00:00 )
May 17, 2024 07:24 UTC
  • Kenya na Uganda zaafikiana kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta

Kenya na Uganda zimekubaliana kujenga kwa pamoja bomba la kusafirishia mafuta kutoka mjini Eldoret katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya hadi Uganda.

Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba hilo, serikali ya Kampala itaweza kuagiza moja kwa moja bidhaa za mafuta yaliyosafishwa kupitia Nairobi.

Rais William Ruto wa Kenya na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni wameshuhudia kusainiwa makubaliano hayo muhimu ya kihistoria jijini Nairobi. Kurefushwa kwa bomba hilo kutoka Eldoret hadi Kampala kunatazamiwa kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na jirani yake Uganda.

Aidha nchi mbili hizo zimesaini makubaliano yanayolifungulia mlango Shirika la Taifa la Mafuta la Uganda, liweze kuagiza bidhaa za petroli kupitia Bandari ya Mombasa.

Rais Ruto wa Kenya amesema kusainiwa makubaliano hayo mjini Nairobi, kunalenga kuhitimisha changamoto za kisheria zinazoikabili Uganda wakati wa kuagiza bidhaa hizo. 

Uganda pia ina mradi wa pamoja wa bomba la mafuta kati yake na Tanzania

Kadhalika Kenya na Uganda zimekubaliana kufanikisha ujenzi wa reli ya mwendo kasi (SGR) kutoka mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru nchini Kenya hadi Uganda, na kisha hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini zimeazimia kuweka nguvu ya pamoja ili kufanikisha ujenzi wa reli ya SGR inayopita Afrika Mashariki.

Dakta Ruto amesema "Kenya na Uganda zina uhusiano uliokita mizizi kutokana na kuwa na historia na utamaduni unaofanana, na pia kutokana na azma yao ya pamoja ya kuwepo na amani na ustawi katika eneo."