Russia yakanusha madai ya kuwaajiri Wakenya katika vita vya Ukraine
-
Russia yakanusha madai ya kuwaajiri Wakenya katika vita vya Ukraine
Russia imekanusha madai kwamba inawaajiri Wakenya kupigana vitani nchini Ukraine, kufuatia ripoti za Huduma ya Kijasusi ya Kitaifa ya Kenya kwamba zaidi ya Wakenya 1,000 kwa sasa wanapigana upande wa Russia katika mzozo huo.
Ubalozi wa Russia jijini Nairobi umesema umebaini "kampeni hatari na ya kupotosha ya propaganda" katika vyombo vya habari vya Kenya kuhusu ushiriki wa Wakenya katika mzozo huo.
Ubalozi wa Russia umesema "unakanusha madai hayo kwa nguvu zote," ukiongeza kwamba mamlaka ya Russia "haijawahi kushiriki katika kuajiri raia wa Kenya kinyume cha sheria katika Vikosi vya Jeshi vya Shirikisho hilo."
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: Ubalozi wa Russia jijini Nairobi "haujatoa visa yoyote kwa Wakenya wanaotaka kusafiri hadi Russia kwa ajili ya kushiriki katika vita hivyo na umekanusha madia ya kuwahimiza kwa namna yoyote Wakenya kushiriki katika vita hivyo."
Ubalozi huo uliongeza kuwa bado uko wazi kwa "mazungumzo yenye kujenga na yasiyo na siasa" na serikali ya Kenya na kusema rasimu ya makubaliano ya pande mbili kuhusu uhamiaji wa wafanyakazi, mipango ya usafiri na ushirikiano kati ya vyombo vya kutekeleza sheria imekuwa ikizingatiwa na mamlaka za Kenya kwa miaka kadhaa.
Kanuusho hilo linakuja baada ya kuweko taarifa kwamba, zaidi ya Wakenya 1,000 wamekwenda kupigana upande wa jeshi la Russia nchini Ukraine. Ripoti ya kijasusi iliyowasilishwa katika bunge la Kenya, ilisema kuwa, wengi wa raia hao walidanganywa ili kusaini mikataba ya kijeshi.
Ripoti hiyo ilieleza kwamba, kuna ushahidi unaoonyesha kuwepo kwa njia iliyopangwa ya uajiri, ambapo mafunzo ya awali ya kiusalama hutolewa kama sifa ya kuajiriwa.