Zuma: Nitapigania haki yangu ya kuwania ubunge Afrika Kusini
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ameapa kupigania kile alichokiita 'haki yake' ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika wiki ijayo.
Jumatatu iliyopita, Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ilitoa hukumu kwamba Zuma hastahiki kugombea katika uchaguzi huo, ikisisitiza kuwa hana sifa za kuwa mgombea kwenye zoezi hilo la kidemokrasia.
Kwenye video iliyotumwa kwenye jukwaa la Youtube na chama chake cha kisiasa cha Umkhonto we Sizwe (MK), Zuma amesema: Majaji wa Mahakama ya Katiba wamefanya maamuzi yanayosema sipasi kufurahia uhuru wangu na demokrasia yangu.
Zuma amesisitiza kuwa, "Nitapigania haki zangu mpaka nchi hii itaafiki kwamba uhuru unapasa kuwa uhuru kwa ukamilifu wake, sio tu kwa baadhi ya watu, na kisha dhulma kwa wengine."
Kesi dhidi ya Zuma ilitokana na uamuzi wa mwezi Machi wa Tume ya Uchaguzi nchini Afrika Kusini wa kumuondoa mwanasiasa huyo katika uchaguzi huo kwa madai kwamba, Katiba inazuia mtu yeyote aliyetumikia kifungo cha miezi 12 au zaidi kushikilia wadhifa wa Ubunge.
Mwaka 2021, Zuma alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi dhidi yake kwa tuhuma za kuhusika na rushwa.
Zuma alitarajia kugombea urais kwa tiketi ya chama cha MK, ambacho alijiunga nacho mwaka jana baada ya kukitupia madongo chama tawala cha African National Congress (ANC) ambacho aliwahi kukiongoza. Tarehe 29 Mei, raia wa Afrika Kusini watapiga kura kuwachagua wajumbe 400 wa Bunge. Mwezi mmoja baadaye, wabunge katika bunge jipya watachagua rais ajaye.