Jun 03, 2024 11:27 UTC
  • Mapigano mapya yaripotiwa katika maeneo kadhaa ya Sudan

Watu kadhaa wanahofiwa kuuawa na kujeruhiwa baada ya kuzuka mapigano mapya kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la waasi wanaojulikana kama Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) katika maeneo tofauti ya Sudan.

Duru za habari zinaarifu kuwa, wimbi hilo jipya la mapigano liliripuka jana Jumapili katika mji mkuu Khartoum, mji wa el-Fasher na pia katika majimbo ya Al Jazirah na White Nile.

Inaarifiwa kuwa, wingu zito la moshi lilionekana kuhanikiza hewani likitoka katika Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Al-Jaili kaskazini mwa Khartoum, kutokana na mapigano hayo.

Aidha ndege za jeshi la Sudan zimeshambulia mikusanyiko ya wapiganaji wa RSF katika kijiji cha Bika, magharibi mwa jiji la Wad Madani, makao makuu ya jimbo la Al Jazirah. 

Habari zaidi zinasema kuwa, watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya nyumba zao kushambuliwa kwa maroketi karibu na mji wa el-Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini.

Mapigano jimboni Darfur

Mapigano hayo mapya yanaripoti huku mashirika ya kitaifa na kimataifa ya misaada ya kibinadamu yakionya kwamba, ongezeko la vizuizi na matatizo yanayokabili misaada ya kibinadamu kwa wahitaji nchini Sudan, yatapelekea kuongezeka vifo vya watu maskini nchini humo.

Makabiliano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya Jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na waasi wa RSF ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo. Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 14,000 na takriban milioni 8.5 kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya Sudan, zimegonga mwamba.

Tags