Wamarekani 3 kizimbani wakihusishwa na jaribio la mapinduzi DRC
Raia watatu wa Marekani na mmoja wa Uingereza ni miongoni mwa makumi ya watu wanaotazamiwa kufikishwa katika Mahakama ya Kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo Ijumaa, wakituhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
Katika taarifa, Meja Patrick Muyembe Nsenyansenya, Msajili wa Mahakama ya Kijeshi ya Gombe amesema watuhumiwa hao 53 wanakabiliwa na mashitaka ya ugaidi na kumiliki silaha za zana za kivita kinyume cha sheria.
Aidha amesema washukiwa hao wanaandamwa na mashitaka mengine kadhaa; yakiwemo ya jaribio la mauaji, kujihusisha na makosa ya jinai, mauaji na kufadhili ugaidi.
Mei 19, vikosi vya jeshi la serikali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vilifanikiwa kuzima jaribio hilo la mapinduzi dhidi ya rais wa nchi hiyo, Felix Tshisekedi.
Jeshi la DRC lililaani jaribio hilo la mapinduzi na kueleza kuwa, lililenga kuyumbisha na kuzusha ukosefu wa uthabiti katika taasisi za uongozi nchini humo. Kadhalika Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) alilaani vikali jaribio hilo la mapinduzi DRC.
Moussa Faki Mahamat amesema AU inafuatilia kwa karibu mambo yanavyoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku akikaribisha habari ya kudhibitiwa wahusika wa jaribio.
Msemaji wa Jeshi la DRC, Brigedia Jenerali Sylvain Ekenge amemtaja mwanasiasa Mkongomani aliyekuwa anaishi Marekani, Christian Malanga kuwa kiongozi wa jaribio hilo la mapinduzi lililotibuliwa. Amesema Malanga aliuawa katika tukio hilo.