Mahakama Kuu Kenya yawaamuru polisi kuacha kutumia ukatili dhidi ya waandamanaji
(last modified Fri, 28 Jun 2024 14:06:14 GMT )
Jun 28, 2024 14:06 UTC
  • Mahakama Kuu Kenya yawaamuru polisi kuacha kutumia ukatili dhidi ya waandamanaji

Mahakama Kuu ya Kenya leo Ijumaa imetoa agizo la kuzuia polisi ya kitaifa kutumia maji ya kuwasha, mabomu ya kutoa machozi, risasi za moto na za mpira pamoja na silaha nyengine dhidi ya waandamanaji wanaopinga Muswada wa Fedha wa mwaka wa 2024.

Agizo hilo la Mahakama Kuu ya Kenya limetolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na wakili Saitabao Ole Kanchory ambapo Jaji Mugure Thande pia amezuia matumizi ya nguvu au aina yoyote ya vurugu dhidi ya waandamanaji.

Jaji Thande amesema, ombi la Ole Kanchory ni la umuhimu kwa raia na kwamba kuna haja ya ombi lake kujibiwa.

Vilivile mahakama hiyo imetoa amri kwa polisi kuacha kujihusisha na mauaji ya kiholela, kukamata watu kinyume cha sheria, kuteka nyara, kuwaweka kizuizini, kutesa, kuwatisha, kuwanyanyasa au hata kuwafanyia vitendo vya kikatili wakati wa maandamano dhidi ya Muswada wa Fedha.

Katika kesi hiyo, Kanchory amesema, polisi wa Kenya wamerejelea tena mbinu za zamani za kuwakamata raia kinyume cha sheria, na hata kuwadhalilisha na kuwatesa.

Kanchory anadai kuwa vijana wanaoandamana maarufu kama Gen Z, bado ni kundi la watu walio hatarini wanaohitaji ulinzi maalumu chini ya katiba ya Kenya kifungu cha 20 na 21.

Jumanne wiki hii, waandamanaji walivamia Bunge la Kenya na kuchoma moto sehemu ya jengo hilo.

Mashirika ya kiraia yametangaza kuwa, watu 53 wameshauawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano hayo huku jiji la Nairobi likiripoti vifo 30.

Makumi ya Wakenya wameuawa katika maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha 2024

Waandamanaji hao wa Kenya sasa wanamtaka Rais wa nchi hiyo, William Ruto, ajiuzulu licha ya uamuzi wake wa kuuondoa muswada tata wa fedha wa 2024 uliokuwa umedhamiria kuongeza ushuru ili kusaidia kupunguza mzigo wa madeni nchini humo.

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ametoa wito wa kufanyika uchunguzi na kuwawajibisha waliohusika na mauaji ya waandamanaji hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, Nairobi.