Tangazo la kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Niger
Baada ya kupita miezi minne, hatimaye serikali ya Marekani imetangaza kwamba karibuni hivi itaondoa vikosi vyake vyote vya kijeshi katika ardhi ya Niger.
Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Washington ilikuwa imeahirisha mara kadhaa zoezi la kuondoa vikosi vyake vya kijeshi kutoka Niger, lakini hatimaye imesalimu amri mbele ya mashinikizo ya serikali na watu wa Niger na kutangaza kwamba karibuni hivi itaondoa vikosi vyake vyote vya kijeshi kutoka katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Kwa kufuta makubaliano ya usalama na Marekani, serikali ya Niger ilitaka kuondolewa kwa wanajeshi wa Washington kutoka nchini humo, na Ikulu ya White House ilitangaza mipango mbalimbali ya kuondoka kwa vikosi vyake vya kijeshi kutoka Niger katika kipindi cha miezi minne iliyopita, lakini hakuna hata mpango mmoja kati ya hiyo ambao ulitekelezwa kivitendo.
Ukweli wa mambo ni kuwa, serikali na wananchi wa Niger wanaamini kuwa, uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika ardhi yao ni kuendelea ukoloni na unyonyaji wa Magharibi na ndio maana wanataka majeshi hayo yaondoke nchini mwao. Hata hivyo Marekani ilikuwa ikidhani kwa kutumia mbinu ya kuakhirisha na kusitasita kutekeleza mpango wa kuwaondoa wanajeshi wake huko Niger asaa ingefanikiwa kuendelea kuvibakisha vikosi vyake katika nchi hiyo ya Kiafrika. Baada ya kuakhirisha mara kadhaa, hatimaye, Jenerali Kenneth Ackman, mmoja wa makamanda wa Jeshi la Anga la Marekani, amesema katika mahojiano na Kanali ya Televisheni ya CBS kwamba, mwishoni mwa wiki hii, wanajeshi wa Marekani waliopo katika "kambi ndogo" wataondoka Niger, na kisha mwezi Agosti, wanajeshi wengine 500 wa Marekani waliopo katika kituo kikubwa cha usimamizi cha Niger wataondoka katika ardhi ya nchi hiyo.
Farid Moradi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema:
“Upinzani dhidi ya kuendelea ukoloni katika nchi za Kiafrika unaofanywa na nchi za Magharibi, zikiwemo Marekani na Ufaransa unazidi kupanuka na kuchukua wigo mpana, na hii inatokana na kuongeza mwamko na uelewa wa watu wa Afrika na kuzingatia zaidi usalama wao na maslahi ya taifa. Kwa maana kwamba, wasiwaruhusu Wamagharibi kupora mali na rasilimali zao na kudai kwa udhalili kabisa kwamba, eti wanadhamini usalama wao.
Hata hivyo, kinachowatia wasiwasi watu na serikali ya Niger zaidi ni kutumiwa kambi za kijeshi za Marekani kama vituo vya kijasusi. Kama inavyosemwa, kituo cha ndege zisizo na rubani kinachojulikana kama "Niger Air Base 201" kilitumika kama kituo kikuu cha shughuli za kijasusi cha Shirika la Kijasusi la Marekani CIA. Ni kwa sababu hiyo, ndio maana miezi minne iliyopita, msemaji wa baraza utawala wa kijeshi nchini Niger alitangaza hatua ya baraza hilo ya kufuta mara moja makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Marekani baada ya karibu miaka 12 tangu kutiwa saini kati ya nchi hizo mbili. Uamuzi na hatua hii ya Niger inachukuliwa kuwa pigo kubwa kwa hadhi, heshima na itibari ya Marekani katika eneo hilo.
Baraza la Utawala la Niger lilichukua hatua ya upande mmoja ya kufuta makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Washington ya mwaka 2012 ikiwa ni siku moja tu baada ya safari ya siku tatu nchini Niger ya maafisa wa ngazi za juu wa Marekani. Pengine Marekani haikufikiria kabisa kwamba ingefedheheshwa na kudhalilishwa na Niger kwa njia hii na hasa kwa vile Baraza la Utawala nchini Niger, linalojulikana kwa jina la "Baraza la Taifa la Ulinzi wa Nchi", baada ya kufuta makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Washington, lilitangaza kuwa, uwepo wa askari wa Marekani nchini Niger ni kinyume cha sheria na kunakinzana na maslahi ya nchi hiyo ya Kiafrika.
Ukweli ni kwamba, Waafrika wanataka uhuru wa kweli na mamlaka juu ya rasilimali zao na kamwe hawataruhusu Wamagharibi, hasa Marekani na Ufaransa ambao ni wakoloni wa jadi kudhibiti hatima ya kujiamulia mambo yao.
Ni kwa muktadha huo, ndio maana kanali Amadou Abdel Rahman, msemaji wa Baraza la Ulinzi wa Kitaifa la Niger, alitoa taarifa na kusema kwamba: Serikali ya Niger, kwa kuzingatia maadili na maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo, imeamua kufuta kwa upande mmoja mkataba wake wa kijeshi na Marekani.
Kwa vyovyote vile, tangazo la Marekani kuondoa askari wake nchini Niger linaonyesha azma thabiti ya serikali na watu wa nchi hiyo ya kukomesha ukoloni wa nchi za Magharibi unaoongozwa na Marekani na kwamba, watu wa Afrika kwa kujua na kuegemea malengo yao kitaifa wanataka kuwa na mamlaka ya usalama na maslahi yao ya taifa.