Siku ya Mashahidi wa Uimara na Umoja wa Kitaifa
-
Siku ya Mashahidi wa Uimara na Umoja wa Kitaifa
Natumai hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kuwa nami katika Makala yetu ya Wiki, ambayo kwa juma hili, itaangazia maadhimisho, ya Siku ya Mashahidi wa Uimara na Umoja wa Kitaifa.
Baadhi ya wakati, vita huwa vinaanza katika medani ya mapambano, lakini hatima yake huamuliwa na mahesabu yanayofanyika kabla ya risasi ya kwanza kufyatuliwa. Baada ya kupita mwaka mmoja, tangu yalipoanza mashambulizi makubwa ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, badala ya kushughulikia zaidi simulizi za matukio, sasa hivi tumepata fursa ya kuchunguza sababu zilizopelekea kufeli na kugonga mwamba malengo ya vita hivyo; vita ambavyo vilikusudiwa kudhoofisha muundo wa nguvu na mamlaka ya Iran, lakini hatimaye vikageuka kuwa mtihani wa kupima mshikamano wa kitaifa, uwezo wa kujijenga upya na nguvu za kimkakati za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Alfajiri ya kuamkia tarehe 13 Juni 2025, wakati mazungumzo kati ya Iran na Marekani yalikuwa yangali yanaendelea huku wachambuzi wengi wa kimataifa wakizungumzia uwezekano wa pande hizo mbili, kufikia makubaliano ya utaratibu mpya wa kushughulikia tofauti zao, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni, kwa msaada wa kiintelijensia na kisiasa wa Marekani, zilianzisha moja ya operesheni kubwa zaidi za kijeshi dhidi ya Iran katika historia ya sasa.
Lengo la awali la operesheni hiyo lilikuwa ni kutoa pigo la kimkakati kwa muundo wa nguvu na mamlaka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwaua makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia, kuteketeza miundombinu ya kiulinzi na kuzusha mshtuko na mtikisiko mkubwa wa kisaikolojia ndani ya jamii ya Iran.
Katika mahesabu ya wapangaji wa vita hivyo, mjumuiko wa hatua zote hizo ilipasa uikutanishe Iran na uhalisia mpya wa kisiasa na kijeshi. Uhalisia ambao, ndani yake mfumo wa Kamandi ya kijeshi umevurugwa, ngao ya kuhofisha hujuma dhidi ya nchi imedhoofika huku Tehran ikilazimika kukubali masharti ambayo huko nyuma haingekuwa tayari katu kuyaridhia.
Hivi sasa mwaka mmoja baadaye, katika kumbukumbu ya kwanza ya vita hivyo, suali kuu linaloulizwa, si vita vilianza anzaje; bali kwa nini, -licha ya Marekani na Israel kuwa na uwezo wa juu kabisa katika vita vya angani, utumiaji wa mifumo ya kisasa zaidi ya kiintelijensia pamoja na ushiriki na usaidizi wa moja kwa moja wa ziliopata kwa madola ya Magharibi-, malengo ya kimkakati ya vita hivyo hayakuweza kufikiwa?
Jibu la suali hilo ndio ufunguo wa kufahamu moja ya mabadiliko muhimu zaidi ya kijiopolitiki ya Mashariki ya Kati katika muongo wa sasa.
Hivyo vilikuwa vita vilivyoanzishwa juu ya msingi wa kosa la kimahesabu. Karibu vita vyote vikubwa vya historia ya zama za sasa, vimeanza hivyo. Kuanzia Vita vya Vietnam hadi uvamizi wa Iraq na Afghanistan; navyo vita vilivyoanzishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 13 Juni 2025 havikutoka nje ya mduara wa kanuni hiyo.
Sehemu muhimu ya tathmini zilizotolewa na matanurifikra ya Magharibi baada ya kumalizika vita inaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni na Marekani zilikuwa zimepanga mkakati wao juu ya dhana kadhaa za msingi wa matarajio.
Kwanza zilidhani kwamba, kuwaua makamanda wakuu wa kijeshi kungeweza kuupoozesha mfumo wa uongozi wa Iran. Pili, zilitarajia kuwa mashambulizi makubwa dhidi ya vituo nyeti vya kijeshi na nyuklia yangepunguza uwezo wa Iran wa kujibu mashambulizi hayo. Lakini tatu, ziliamini kwamba, mashinikizo ya kijeshi na ya kisaikolojia ya wakati mmoja yangeshadidisha migawanyiko na mipasuko ya ndani na kuiweka jamii ya Iran katika hali ya kutapatapa.
Ukweli ni kuwa, wapangaji wa vita hivyo walitegemea zaidi taswira waliyojijengea wao wenyewe vichwani mwao kuhusu Iran kuliko kuifahamu Iran halisi ikoje. Mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi, Trita Parsi, alisisitiza katika mahojiano aliyofanyiwa na CNN kwamba Israel “iliudogosha uwezo wa Iran wa kujipanga upya na kukarabati haraka Kamandi yake.”
Mtihani mkubwa wa uongozi na udhibiti wa hali mbaya inayojitokeza katika saa za mwanzo za vita huwa ni miongoni mwa nyakati zenye taathira kubwa zaidi inayoainisha mwelekeo wa vita hivyo. Mauaji ya makamanda wakuu wa kijeshi katika nchi yoyote ile yanaweza kusababisha mparaganyiko katika mnyororo wa kamandi, kuchelewesha uchukuaji maamuzi muhimu na hata kuzusha hali ya mchafukoge.
Ndiyo maana wimbi la kwanza la mashambulizi ya utawala wa Kizayuni lilijikita zaidi katika kufikia lengo hilo.
Kilichojiri baadaye kilikuwa moja ya sababu muhimu zaidi zilizopelekea kufeli malengo ya awali ya vita hivyo.
Muda mfupi tu baada ya kuuawa shahidi makamanda wakuu wa kijeshi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, aliwateua makamanda wapya wa kushika nyadhifa zao. Hatua hiyo ilikuwa na ujumbe muhimu wa kimkakati, nao ni kwamba muundo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu haujajengwa kwa kutegemea watu binafsi, bali umepangwa na kuratibiwa kitaasisi, na kwa kutegemea tajiriba na uzoefu wa muda mrefu pamoja na mifumo ambayo ilisharatibiwa tokea hapo kabla.
Hapo baadaye, wataalamu wengi wa kijeshi wa Magharibi walikuja kukiri kuwa, kasi ya kujengwa upya Kamandi ya kijeshi nchini Iran ilikuwa kubwa kuliko makadirio ya awali yaliyofanywa na maadui.
Hali hiyo iliufanya utawala wa Kizayuni ushindwe kutumia pengo lililosababishwa na mauaji ya makamanda hao kufikia malengo yake ya kuzusha machafuko na kuporomoka mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mwenendo wa matukio yaliyojiri baada ya vita ulienda kinyume kabisa na dhana na matarajio ya Wazayuni na mabwana zao Marekani.
Mafanikio muhimu zaidi ya Iran katika vita hivyo hayakupatikana katika medani ya kijeshi, bali ni katika uga wa kijamii.
Wapangaji wa vita walidhani kwamba mashambulizi makubwa, mauaji ya ulengaji watu maalumu na mashinikizo ya kisaikolojia vingeweza kusababisha migawanyiko na mifarakano na kuiyumbisha jamii ya Iran. Hata hivyo, kilichotokea, kilikuwa kinyume kabisa na matarajio yao.
Historia ya Iran imeonyesha kuwa, kila pale mamlaka ya umoja wa ardhi yote na usalama wa taifa vilipokabiliwa na vitisho kutoka nje, mipasuko ya kisiasa na kijamii ilififia liliposimama neno “Iran” mbele ya macho ya wananchi.
Vita vya kulazimishwa vya siku 12 vilidhihirisha tena ukweli huo wa kihistoria.
Kuanzia mirengo ya kisiasa yenye mielekeo tofauti mpaka matabaka mbalimbali ya ndani ya jamii, yote hayo yalijenga hisia za pamoja na za aina moja: ambazo ni kuilinda nchi kwa kukabiliana na uchokozi wa kigeni.
Kuuawa shahidi zaidi ya Wairani 1,100, wakiwemo makamanda wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, askari wa vikosi vya ulinzi pamoja na raia wa kawaida, kuligeuka kuwa msingi wa kujengeka kumbukumbu ya pamoja katika upeo wa kitaifa.
Wale wote waliouawa shahidi wakawa alama na nembo za Muqawama na kusimama kidete kitaifa.
Kubadilisha mlingano wa Ngao ya Kuhofisha Hujuma kabla ya vita vya Juni13, 2025, ilikuwa sehemu muhimu ya misamiati ya kiusalama ya Magharibi iliyotilia mkazo, kuwa na nguvu za kipekee utawala wa Kizayuni za ngao ya kuhofisha hujuma.
Lakini vita vya siku 12 vilitoa changamoto kubwa kwa nyingi kati ya dhana zilizokuwa zimejengeka juu ya mtazamo huo.
Kwa mara ya kwanza katika upeo huo, vituo vya kijeshi, vya kitaalamu na vya teknolojia vya Israel vililengwa kwa mashambulizi ya moja kwa moja.
Picha na klipu zilizosambazwa, zilizoonyesha makombora yakipiga baadhi ya maeneo nyeti, zilizishangaza na kuziacha vinywa wazi duru nyingi za kiusalama za Magharibi.
Ukweli ni kwamba vita hivyo vilionyesha kuwa hata mifumo ya kiulinzi ya utunguaji makombora ya utaalamu wa juu kabisa haiwezi kutoa kinga kamili na ya asilimia mia moja.
Mabadiliko hayo yalikuwa na athari muhimu za kimkakati kwa eneo zima.
Nchi nyingi za Mashariki ya Kati zilibaini kuwa enzi za ubabe wa kijeshi wa upande mmoja zimeshakaribia ukingoni, na milingano ya kiusalama ya kikanda imeingia katika awamu mpya.
Kujiingiza moja kwa moja Marekani katika vita kupitia mashambulizi iliyofanya dhidi ya vituo vya Iran vya mpango wa amani wa nyuklia ilikuwa hatua nyingine muhimu sana ya mabadilio katika mgogoro huo.
Washington ilidhani kwamba hatua hiyo ingeweza kubadilisha mizani ya vita kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni.
Hata hivyo, majibu ya Iran ya kuitwanga kambi ya kijeshi ya Al Udeid nchini Qatar yalionyesha kuwa ushiriki wowote wa moja kwa moja wa Marekani katika vita ungekuwa na gharama kubwa kwa maslahi yake katika eneo.
Jambo hilo ndilo lililowafanya wachambuzi wengi wa Magharibi watoe indhari juu ya hatari ya vita hivyo kuenea katika eneo lote la Mashariki ya Kati.
Wasiwasi wa kuvurugika usafirishaji wa nishati, kuwepo tishio dhidi ya njia za usafiri wa baharini pamoja na uwezekano wa kuingia kwenye mapigano pande zingine mpya, ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi zilizoongeza mashinikizo ya kuhitimishwa vita.
Marekani na utawala wa Kizayuni hazikuweza kufikia malengo yao makuu. Iran haikusalimu amri. Muundo wa Kamandi ya kijeshi haukusambaratika. Uwezo wa makombora haukuangamizwa. Na mshikamano wa ndani wa kitaifa haukudhoofika.
Lakini muhimu zaidi ni kwamba vita hivyo havikuweza kugeuzwa kuwa wenzo wa kuzidisha mashinikizo ya ndani dhidi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Katika hali kama hiyo, kuendelea kwa vita kungezisababishia Marekani na utawala wa kizayuni gharama na hasara zisizoweza kutabirika.
Kwa sababu hiyo, usitishaji vita liligeuka kuwa chaguo lisiloweza kuepukika.
Funzo muhimu zaidi la vita vya kulazimishwa vya siku 12 lilikuwa ni kushindwa maadui kuitambua nchi, jamii na mfumo wa kisiasa unaotawala Iran.
Marekani na utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine tena zilifanya makosa ya kimahesabu katika tathmini yao kuhusu Iran.
Wao walizipima nguvu za Iran katika uga wa makombora, vituo vya kijeshi na makamanda wake, ilhali chanzo muhimu zaidi cha nguvu za Iran kinatokana na vitu vingine; ambavyo ni kumbukumbu za kihistoria za taifa, uzoefu na tajiriba ya Muqawama, uwezo wa kujenga upya taasisi zake, na uwezo wa jamii yake wa kugeuza vitisho vya nje kuwa chachu ya kuimarisha mshikamano wa ndani.
Baada ya kupita mwaka mmoja tangu vilipoanzishwa vita vya siku 12, athari nyingi za kimaada za uchokozi huo zingali zinaonekana, kwa familia za Mashahidi kuendelea kuwaomboleza wapendwa wao.
Pamoja na hayo, kilichobaki zaidi kwenye kumbukumbu za historia za taifa la Iran ni simulizi ya kushindwa njama iliyokuwa na dhamira ya kuidhoofisha Iran, kwa hatimaye kuishia kuwa chachu ya uimara wa kitaifa na mshikamano wa kijamii.
Na ndiyo maana katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tarehe 23 Khordad, inayosadifiana na Juni 13, ni nembo ya siku ambayo taifa la Iran lilisimama imara mbele ya moja ya mitihani migumu zaidi katika historia yake ya zama za sasa, na kuonyesha kwamba nguvu halisi za mataifa hazipatikani kwenye maghala ya silaha pekee, bali pia katika mshikamano wa kitaifa, azma ya pamoja ya kulinda uhuru na mamlaka ya taifa.
Wachambuzi wengi walidhani kwamba mafunzo yaliyopatikana kutokana na vita vya siku 12 vya Juni 2025 yangezifanya Washington na Tel Aviv zitathmini upya muelekeo wao kuhusu Iran.
Hata hivyo, mwenendo wa matukio yaliyofuata ulionyesha kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kiusalama wa Magharibi walikuwa wangali na mitazamo yao ileile ya awali kuhusu Iran.
Katika uchokozi mpya wa kijeshi ulioanzishwa dhidi ya Iran mwaka 2026, kwa mara nyingine kulikuwepo na dhana kwamba mashinikizo ya nguvu kubwa za kijeshi yanaweza kuiweka Tehran kwenye nafasi ya udhaifu na kubadilisha mizani ya nguvu kwa manufaa ya Marekani na utawala wa Kizayuni.
Lakini mara hii, jibu la Iran halikuwa la vipigo vya kawaida tu vya kijeshi.
Tehran ilihakikisha inabadilisha kanuni za mchezo kwa kuupanua uwanja wa mapigano kutoka kwenye hali ya vita vyenye mpaka vya baina ya pande mbili na kuwa mgogoro wenye wigo mpana wa kikanda na kimataifa.
Mabadiliko muhimu zaidi yaliyoshuhudiwa ni tathira za moja kwa moja za vita hivyo kwa usalama wa nishati duniani.
Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao kwa miaka mingi umekuwa ukitambulika kama moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa nishati duniani, kwa mara nyingine uligeuka kuwa kitovu cha kuainisha hatima ya uchumi wa dunia.
Karibu khumsi, yaani moja ya tano ya biashara ya mafuta duniani na kiasi kikubwa cha mauzo ya gesi asilia iliyoyeyushwa husafirishwa kupitia njia hiyo.
Kwa sababu hiyo, tishio lolote dhidi ya usalama wa njia hiyo ya baharini haliishii kuwa suala la kikanda tu, bali hubadilika haraka kuwa mgogoro wa kimataifa.
Kile ambacho Marekani na utawala wa Kizayuni zilikipuuza katika mahesabu yao ni ukweli huo wa kijiopolitiki.
Wao walivitathmini vita kwa kupima uwezo wa kijeshi tu wa pande mbili, ilhali Iran ina uwezo mkubwa wa kijiopolitiki na kiuchumi ambao unaweza kueneza athari za mzozo wowote ule hadi nje ya mipaka ya eneo.
Katika dunia ambayo uchumi wa mataifa umefungamana pamoja kwa kiwango kikubwa, mgogoro wa kiusalama katika Ghuba ya Uajemi unaweza kueneza athari zake kuanzia kwenye masoko ya nishati ya Asia hadi vituo vya miamala ya fedha vya Ulaya na Marekani.
Funzo muhimu zaidi la vita viwili vilivyoanzishwa dhidi ya Iran ndani ya kipindi cha miezi tisa linapasa kuchunguzwa katika kushindwa tena na tena kwa ufahamu mmoja wa kimkakati; ufahamu wa kudhani, inawezekana kubadilisha kwa upande mmoja milingano ya kisiasa na kiusalama ya eneo kwa kutegemea uwezo wa juu tu zaidi wa kijeshi.
Tajiriba ya mwaka 2025 na 2026 imeonyesha kuwa Iran inao uwezo wa kuhimili mashinikizo ya kijeshi, na ina uwezo pia wa kupanua wigo na ukubwa wa mapigano na mzozo wowote ule na kuzifanya gharama zake zivuke mipaka ya eneo.
Kwa mtazamo huo, “Siku ya Mashahidi wa Uimara wa Kitaifa na Umoja wa Kitaifa” ni alama ya funzo muhimu la kimkakati kwa eneo na dunia kwa ujumla.
Siku hii inakumbusha kuwa katika Mashariki ya Kati, hakuna vita vyovyote vitakavyoanzishwa dhidi ya Iran ambavyo vitaweza kubaki kuwa vya mipaka maalumu; na kosa lolote la kimahesabu litakalofanywa kuhusiana na Iran litasababisha madhara makubwa, si kwa waanzishaji vita tu, bali kwa eneo zima na hata kwa uchumi wa dunia…/