Algeria yasimamisha matamasha ya sanaa kuiunga mkono Gaza
(last modified Sat, 13 Jul 2024 11:37:02 GMT )
Jul 13, 2024 11:37 UTC
  • Algeria yasimamisha matamasha ya sanaa kuiunga mkono Gaza

Wizara ya Utamaduni ya Algeria imetangaza kusimamisha matamasha yote makubwa ya sanaa katika msimu huu wa joto kali, kuonyesha mshikamano na wananchi madhulumu wa Wapalestina wanaoendelea kuuawa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Soraya Mouloudji, Waziri wa Utamaduni wa Algeria amesema wizara hiyo badala ya kusimamia matamasha hayo, itaongeza harakati na shughuli za kutangaza na kuonyesha uungaji mkono wa taifa hilo kwa wananchi wa Palestina hasa wa Ukanda wa Gaza.

Ameeleza bayana kuwa, uamuzi huo wa kusimamisha matamasha yote makubwa ya sanaa katika msimu huu wa joto kali nchini humo umetokana na msimamo wa jadi na usiotetereka wa Algeria wa kuunga mkono kadhia ya Palestina, na mapambano halali ya Wapalestina dhidi ya utawala katili wa Israel.

Mwishoni mwa mwaka uliopita pia, Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya Algeria ilitangaza kuakhirishwa shughuli zote za kitamaduni na matamasha kote nchini humo, ikiwa ni pamoja na Tamasha la Filamu la Annaba la Mediterania ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika Novemba 3 hadi 9 mwaka jana.

Israel inaendeleza mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Gaza ikisaidiwa kwa hali na mali na Marekani

Algeria ni miongoni mwa mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kupaza sauti na kufanya maandamano ya kuliunga mkono taifa la Palestina; na kulaani jinai za Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa nchi hiyo.

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria sanjari na kutoa mwito wa kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, alisisitiza hivi karibuni kuwa, utawala wa Kizayuni hautilii maanani hata kidogo Umoja wa Mataifa na unapuuza yale yanayoidhinishwa na taasisi hiyo na kukiuka wajibu na majukumu yake.