Ethiopia: Bara la Afrika lina hamu ya kujiunga na BRICS
Spika wa Bunge la Ethiopia amesema aghalabu ya nchi za Afrika zina hamu ya kuwa wanachama wa kundi la BRICS la mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani.
Agegnehu Teshager amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Russia Today pambizoni mwa Mkutano wa 10 wa Jukwaa la Kibunge la BRICS mjini St. Petersburg nchini Russia na kusisitiza kuwa: Akthari ya nchi za Afrika zimeonyesha hamu ya kuwa wanachama wa BRICS.
Spika wa Bunge la Juu la Ethiopia amesema: Uchumi wa Ethiopia unastawi kwa kasi kubwa. Tuna fursa kubwa ya kupanua uchumi (wa BRICS). Ethiopia ni lango la BRICS la kuingia barani Afrika; Afrika ni fursa nzuri kwa jumuiya hiyo ya kiuchumi.
Kadhalika amekosoa muundo wa sasa wa nidhamu ya dunia, na kuutaja kuwa usio wa kiadilifu. Amesema, "Dunia hivi sasa haina uadilifu, kama unavyofahamu, kuanzia muundo wa Umoja wa Mataifa hadi Baraza la Usalama la umoja huo.
Spika wa Bunge la Ethipia amesisitiza kuwa: Kuna taasisi nyingi za kimataifa duniani hivi sasa, kwa hivyo BRICS ni jukwaa mbadala kwa nchi wanachama.
Kundi hili la BRICS ambalo hadi hivi karibuni lilikuwa na wanachama wakuu watano tu, yaani Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, lililipanuka zaidi Januari mwaka huu baada ya Iran, Ethiopia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu kujiunga na kundi hilo.