Jul 18, 2016 08:10 UTC
  • Kuanza utekelezaji wa mpango wa kuwapokonya silaha waasi DRC

Mpango wa kuwapokonya silaha waasi walioko katika mkoa wa Ituri huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeanza kutekelezwa.

Lengo la kutekelezwa mpango huo ni kurejesha amani na utulivu katika maeneo yenye ghasia na machafuko kama Mambasa na kusini mwa Irumu kwenye mkoa wa Ituri. Mpango huo pia itahusu kupokonywa silaha waasi walioko katika maeneo mengine ya mbali. Wasimamizi wa mpango huo wanasema, waasi watakaokabidhi silaha zao watarejeshwa katika maisha ya kawaida.

Suala la kuyapokonya silaha makundi ya waasi na yenye silaha daima limekuwa tatizo kubwa kwa nchi za Kiafrika zilizokumbwa na migogoro baada ya kumalizika vita na machafuko ya ndani. Mkoa wa Ituri huko kaskazini mashariki mwa Congo umekuwa katika ghasi na machafuko kwa kipindi cha miongo miwili sasa kutokana na uwepo wa makundi mengi ya waasi katika eneo hilo na vilevile mizozo ya mara kwa mara kati ya makundi na makabila hasimu. Mizozo ya kikabila kati ya kaumu za Lendu na Hema na mapigano kati ya makundi mbalimbali ya waasi kwa ajili ya kudhibiti migodi yenye utajiri wa madini ya dhahabu na almasi ni miongoni mwa sababu za machafuko na ukosefu wa amani katika eneo hilo. Pamoja na hayo wachambuzi wa mambo wanasisitiza kuwa, kushindwa serikali ya Kinshasa kudhibiti hali ya mambo katika maeneo ya kati na kaskazini mwa nchi kunachangia katika ghasia na machafuko yanayoendelea kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo. Vilevile harakati za kutaka kujitenga katika mikoa ya Katanga na Kasai ni miongoni mwa sababu zinazozidisha machafuko na ukosefu wa amani huko kaskazini na mashariki mwa Congo.

Wakati huo huo uingiliaji wa nchi za Uganda wa Rwanda katika masuala ya eneo la mashariki mwa nchi hiyo na uungaji mkono wao kwa baadhi ya makundi ya kikaumu vinaathiri sana katika machafuko hayo. Itakumbukwa kuwa, nchi za Rwanda na Uganda ambazo ni majirani wa mashariki wa Congo zilichangia katika kuanzisha vita vilivyozishirikisha nchi kadhaa ndani ya nchi hiyo. Vita hivyo vya pili vya Congo vilivyotokea kati ya mwaka 1998 na 2003 vilipewa jina la Vita vya Kwanza vya Dunia vya Afrika kutokana na kushirika karibu nchi nane katika vita hivyo.

Kwa sasa utekelezaji wa mpango wa kuyapokonya silaha makundi ya waasi katika mkoa wa Ituri ni fusra nzuri ya kukomesha mgogoro wa mashariki mwa Congo. Hata hivyo inatupasa pia kuelewa kuwa, suala la kuwapokonya silaha waasi na makundi hasimu peke yake halitoshi bali ni muhimu pia kwa nchi 9 majirani na Congo kijiepusha suala la kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi hiyo, la sivyo juhudi za sasa hazitazaa matunda yanayokusudiwa.

Tags