Usalama waimarishwa zaidi Nairobi Kenya huku mkutano wa UNCTAD ukiendelea
Usalama umeimarishwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi huku mkutano wa 14 wa Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ukiendelea kufanyika mjini humo.
Ripoti zinaeleza kuwa, vyombo vya usalama vya Kenya vimeimarisha usalama katika jiji la Nairobi baada ya kuenea tetesi kwamba, kuna watu 11 wenye silaha ambao wanafungamana na kundi la kigaidi la al-Shabab la Somalia wanaojiandaa kufanya mashambulio wakati wa kufanyika mkutano huo.
Kufuatia taarifa hizo vyombo vya usalama vya Kenya vimesema haviwezi kupuuza tishio hilo ambalo yumkini likatekelezwa kivitendo.
Mkutano huo unahudhuriwa na wajumbe zaidi ya 10,000 kutoka nchi 194 duniani ambao wanafanya jitihada za kuhakikisha kwamba sera za kieneo na kimataifa zinachangia katika maendeleo endelevu.
Mkutano wa 14 wa Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ulioanza jana Jumapili unatarajiwa kumalizika Ijumaa ijayo ya tarehe 22 mwezi huu.
Baadhi ya barabara katika jiji la Nairobi zimefungwa kufuatia kufanyika mkutano huo hali ambayo imesababisha adha na usumbufu kwa wakazi wa jiji hilo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano wa dunia kwa ajili ya kutimiza malengo ya kijamii na kiuchumi yaliyoainishwa na nchi za dunia.