Waliokufa kutokana na mvua, mafuriko Sudan wapindukia 50
(last modified Sun, 11 Aug 2024 07:34:36 GMT )
Aug 11, 2024 07:34 UTC
  • Waliokufa kutokana na mvua, mafuriko Sudan wapindukia 50

Watu zaidi ya 50 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko katika maeneo mbali mbali ya Sudan.

Wizara ya Afya ya Sudan ilisema jana Jumamosi kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mvua, mafuriko na maporomoko ya ardhi katika majimbo kadhaa hasa ya kaskazini mwa Sudan imefikia 53.

Idara ya Dharura ya Wizara ya Afya ya Sudan imenukuliwa na shirika la habari la Xinhua ikisema kuwa, mbali na watu 53 kupoteza maisha kutokana na majanga hayo ya kimaumbile, wengine zaidi ya 208 wamejeruhiwa, huku familia 9,777 zikiathirika. Majimbo tisa ya Sudan yameathiriwa na mvua hizo zilizosababisha mafuriko yaliyobomoa kikamilifu nyumba 2,000, huku nyingine zaidi ya 4,000 zikibomolewa kwa kiasi fulani.

Jumatatu iliyopita, Wizara ya Afya ya Sudan ilitangaza vifo vya watu 32 na kujeruhiwa wengine 107 kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika majimbo 7 ya nchi hiyo tangu mwezi wa Juni. 

Mafuriko Sudan

Siku mbili baadaye, shirika rasmi la Habari la Sudan (SUNA) liliripoti kuwa watu 11 wamefariki dunia na wengine 60 kujeruhiwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko katika mji wa Abu Hamad kaskazini mwa Sudan

Maafa ya mafuriko mwaka huu yanaambatana na kuendelea kwa mateso yaliyosababishwa na vita kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF, ambavyo tangu viaanze Aprili mwaka 2023, takriban watu 18,800 wameuawa, huku wengine karibu milioni 10 wakilazimika kukimbia makazi yao.