Mafuriko yaua zaidi ya watu 50 kaskazini mwa Chad
(last modified Fri, 16 Aug 2024 10:39:01 GMT )
Aug 16, 2024 10:39 UTC
  • Mafuriko yaua zaidi ya watu 50 kaskazini mwa Chad

Watu wasiopungua 54 wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika jimbo la Tibesti la kaskazini mwa Chad.

Hayo yametangazwa na mamlaka na vyombo vya habari vya nchi hiyo ambavyo vimeeleza kuwa, zaidi ya watu 50,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mafuriko katika jimbo hilo.

Mahamat Tochi Chidi, Gavana wa mkoa wa Tibesti alinukuliwa na shirika la habari la Xinhua jana Alkhamisi akisema kuwa, mvua hiyo iliyoanza Ijumaa iliyopita na kuendelea hadi juzi Jumatano imeharibu mali na miundomsingi mbali na kusababisha mauti.

Naye Fatime Boukar Kossei, Waziri wa Masuala ya Jamii, Mshikamano wa kitaifa na masuala ya kibinadamu wa Chad amesema kwamba, makazi ya muda yamejengwa kwa ajili ya kuwahifadhi watu waliohama makazi yao.

Chad imekumbwa na mafuriko tangu katikati ya Mei mwaka huu, janga la kimaumbile ambalo tayari limeathiri watu zaidi ya 245,000, kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA.

Shirika hilo la UN liliripoti wiki iliyopita kuwa, mvua hizo pamoja na mafuriko makubwa tayari yameshasababisha vifo vya watu 40 katika nchi hiyo iliyoko katika makutano ya maeneo ya katikati na kaskazini mwa Afrika.

Tags