Familia 1,200 zahama makazi yao kutokana na mafuriko Khartoum, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131650-familia_1_200_zahama_makazi_yao_kutokana_na_mafuriko_khartoum_sudan
Zaidi ya familia 1,200 za Sudan zimefurushwa katika nyumba zao na mafuriko katika mji wa Bahri katika jimbo la Khartoum, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema hayo jana Jumapili.
(last modified 2025-10-06T07:15:02+00:00 )
Oct 06, 2025 07:15 UTC
  • Familia 1,200  zahama makazi yao kutokana na mafuriko Khartoum, Sudan

Zaidi ya familia 1,200 za Sudan zimefurushwa katika nyumba zao na mafuriko katika mji wa Bahri katika jimbo la Khartoum, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema hayo jana Jumapili.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema katika taarifa kwamba, mafuriko hayo yameharibu kikamilifu nyumba tano na kuacha nyumba nyingine nyingi zikiharibia kwa kiasi fulani.

Shirika hilo limesema familia nyingi zimeondoka eneo hilo wakihofia uharibifu tarajiwa wa mafuriko, huku wale waliohamishwa wakitafuta makazi ndani ya jamii zinazowapokea katika eneo hilo.

Mikoa kadhaa nchini Sudan imekumbwa na mafuriko kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji ya Mto Nile na vijito vyake; Nile Nyeupe, ambayo yanatiririka kutoka Ziwa Victoria, na Blue Nile, ambayo yanatoka nyanda za juu za Ethiopia.

Zaidi ya watu 125,000 wameathiriwa na mvua na mafuriko nchini Sudan tangu Juni 30, kwa mujibu wa takwimu za serikali. Sudan kwa kawaida hupata mvua kubwa wakati wa msimu wa mvua, kuanzia Juni hadi Oktoba, ambayo mara nyingi husababisha mafuriko ya kila mwaka.

Katika nchi jirani ya Sudan Kusini, mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa  yameripotiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 20 na kuathiri wengine karibu 640,000 katika kaunti 26 katika majimbo sita ya nchi hiyo, hayo yamesemwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA).

Ripoti hiyo imekuja siku moja baada ya shirika la misaada ya kimataifa la Save the Children kusema kuwa, takriban watu milioni 1.4 nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na tishio la mafuriko mwaka huu, huku kukiwa na utabiri wa mvua nyingi katika mwezi huu wa Oktoba na Novemba.