Makumi waaga dunia kwa mafuriko nchini Niger, maelfu waathirika
Kwa uchache watu 47 wamepoteza maisha, huku zaidi ya 56,000 wakilazimika kuhama makazi yao kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha hivi majuzi nchini Niger.
Kwa mujibu wa Mamlaka Kuu ya Ulinzi wa Raia, mafuriko hayo yameathiri familia 7,754 katika vitongoji na vijiji 339 vya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
"Takriban watu 30 waliaga dunia baada ya nyumba zao kuporomoka huku 17 wakifa maji. Aidha, mafuriko hayo yamepelekea kujeruhiwa watu 70 na kusababisha vifo vya mifugo kama ng'ombe 257," kurugenzi hiyo imesema katika taarifa yake ya jana Jumatano.
Kamati ya kitaifa yenye jukumu la kuzuia athari za mafuriko imesema imeanza kusambaza chakula cha msaada, ikilenga familia 3,776. Serikali imetenga faranga za CFA bilioni 12 (dola milioni 21.3) kusaidia familia na watu binafsi walioathiriwa na mafuriko kote nchini, kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo.
Habari zaidi zinasema kuwa, mvua hiyo imesababisha uharibifu mkubwa na kusomba nyumba na miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara na madaraja. Mwaka jana 2024, mvua kubwa iliathiri karibu watu milioni 1.5 katika mikoa yote minane ya Niger.
Mabadiliko ya tabianchi yametajwa kusababisha hali hiyo nchini Niger, ingawa baadhi ya wananchi wamesema sababu za kibinadamu pia zimechangia.
Mafuriko yameibuka kuwa moja ya majanga ya kimaumbile hatari zaidi ulimwenguni, huku Afrika ikiwa mhanga mkubwa zaidi wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa.