Sudan yatangaza janga la kipindupindu baada ya mvua kubwa kunyesha nchini humo
(last modified 2024-08-18T07:04:53+00:00 )
Aug 18, 2024 07:04 UTC
  • Sudan yatangaza janga la kipindupindu baada ya mvua kubwa kunyesha nchini humo

Waziri wa Afya wa Sudan ametangaza janga la kipindupindu nchini humo baada ya mvua kubwa kunyesha kwa wiki kadhaa.

Haitham Ibrahim amesema: "Tunatangaza janga la ugonjwa wa kipindupindu kwa sababu ya hali mbaya ya hewa na kuchafuka kwa maji ya kunywa."

Haitham Ibrahim, Waziri wa Afya wa Sudan 

Amesema, wamechukua uamuzi huo kwa kushauriana na mamlaka husika katika jimbo la Kassala mashariki mwa Sudan baada ya maabara ya afya ya umma kugundua vijidudu maradhi vya kipindupindu.

Nchi hiyo ya kaskazini-mashariki mwa Afrika imekumbwa na vita tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan chini ya mtawala mkuu wa nchi hiyo, Abdel Fattah al-Burhan, na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), kinachoongozwa na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo.

Ugonjwa wa kipindupindu unaweza kusababisha kupungukiwa pakubwa maji mwilini kutokana na kuhara sana ambapo baadhi ya wagonjwa hupoteza maisha katika kipindi cha masaa kadhaa tu. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa kesi za kipindupindu 307,433 na vifo 2,326 vimeripotiwa katika nchi 26 hadi kufikia Julai 28 mwaka huu. 

Tags