Bwawa laporomoka na kuua watu zaidi ya 60 nchini Sudan
(last modified 2024-08-26T11:04:42+00:00 )
Aug 26, 2024 11:04 UTC
  • Bwawa laporomoka na kuua watu zaidi ya 60 nchini Sudan

Kwa akali watu 60 wameripotiwa kufariki dunia baada ya bwawa moja kuvunjika huko mashariki mwa Sudan kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini humo.

Gazeti la Sudan la Al-Taghyeer limeripoti leo Jumatatu kuwa, watu wengi bado hawajulikani walipo baada ya Bwawa la Arbat kuporomoka, ambalo lina hifadhi ambayo ni chanzo kikuu cha maji safi kwa wakazi wa mji wa Port Sudan.

Gazeti hilo, likinukuu mashuhuda, limesema mafuriko yamesomba vijiji vilivyoko karibu na Bwawa la Arbat, na kugonga milima inayovizunguka na kisha kurudi kwenye vijiji na kusababisha uharibifu mkubwa.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti kuwa, mamia ya wakaazi wa vijiji hivyo wamekimbilia nyanda za juu na kwenye maeneo ya milima ili kuepuka hatari ya mafuriko, huku wengine wakisalia wamekwama na kushindwa kuondoka kwenye vijiji hivyo.

Makumi ya watu wamefariki dunia na mamia ya wengine wamejeruhiwa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko na mapromoko ya ardhi katika maeneo mbali mbali ya Sudan.

Wiki iliyopita, Haitham Ibrahim, Waziri wa Afya wa Sudan alitangaza janga la kipindupindu nchini humo baada ya mvua kubwa kunyesha kwa wiki kadhaa mfululizo.

Tags