Sep 16, 2024 12:03 UTC
  • Watu 40 wauawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa RSF Sudan

Makumi ya raia wameuawa katika shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika kijiji kimoja katikati mwa Sudan.

Kamati ya Mapambano ya Abu Gouta, ambalo ni kundi lisilo la kiserikali, imesema katika taarifa kuwa, "Shambulio la RSF kwenye kijiji cha Gouz Al-Naqa eneo la Abu Gouta katika jimbo la al-Jezira liliua takriban raia 40."

Maiti kadhaa zimetapakaa kijijini kufuatia shambulio hilo la jana Jumapili, huku RSF ikizuia wanakijiji waliohamishwa kurudi kuizika miili hiyo.

Kamati hiyo imetoa wito kwa mashirika ya kiraia kuishinikiza RSF iruhusu wakazi kuingia kijijini humo na kuwazika raia hao waliouawa.

Haya yanajiri wiki moja baada ya raia wengine wasiopungua 21 kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya wanamgambo wa RSF kuvurumisha makombora sokoni katika mji wa Sinnar katikati mwa Sudan.

Jeshi la Sudan (SAF) linapigana vita na Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF) tangu katikati ya Aprili mwaka jana; ambapo hadi sasa watu zaidi ya elfu 20 wameuawa vitani na wengine karibu ya milioni 10 wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi jirani. 

Tags