Somalia yajiunga na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia
Somalia imejiunga na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika Mkutano Mkuu wa wakala huo ulioanza jana Jumatatu mjini Vienna.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia imesema katika taarifa siku ya Jumatatu kuwa: Huu ni wakati muhimu kwa nchi yetu, kuangazia kujitolea kwetu kwa ushiriki wa amani wa nyuklia na maendeleo endelevu,"
Naye Waziri wa Habari wa Somalia, Daud Aweis amesema Somalia kama mwanachama wa IAEA, inatarajia kushirikiana na jamii ya kimataifa kutumia teknolojia ya nyuklia kwa manufaa ya taifa hilo na kuhakikisha viwango vya juu vya usalama wa nishati hiyo.
Mkutano Mkuu wa 68 wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) ulianza jana Jumatatu mjini Vienna, Austria kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa nchi 179 duniani.
Somalia ndiye mwanachama mpya zaidi na wa 179 wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuratibu na kusimamia nyuklia.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) amesema kuwa, kuzingatiwa usalama wa nishati ya nyuklia ni moja ya vipaumbela vya wakala huo.