Shrika la Muhuri: Kenya inakabiliwa na tatizo kubwa la mauaji ya kiholela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11650-shrika_la_muhuri_kenya_inakabiliwa_na_tatizo_kubwa_la_mauaji_ya_kiholela
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Muslims for Human Rights (Muhuri) nchini Kenya, Hassan Abdi Abdille amesema kuwa, wimbi la kutoweka kwa watu na kisha kupatikana baadaye wakiwa wameuawa kikatili, limekuwa sugu na kwamba serikali haijachukua hatua za kisheria kuhusu suala hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2016 23:56 UTC
  • Shrika la Muhuri: Kenya inakabiliwa na tatizo kubwa la mauaji ya kiholela

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Muslims for Human Rights (Muhuri) nchini Kenya, Hassan Abdi Abdille amesema kuwa, wimbi la kutoweka kwa watu na kisha kupatikana baadaye wakiwa wameuawa kikatili, limekuwa sugu na kwamba serikali haijachukua hatua za kisheria kuhusu suala hilo.

Abdille aliyasema hayo jana  wakati wa uzinduzi wa ripoti ya shirika la kutetea haki za kibinadamu kimataifa la Human Rights Watch (HRW) na kusema kama ninavyomnukuu: "Ninataka kumwambia Rais kwamba, yuko hatarini kuweka historia mbaya kuhusiana na suala la kutoweka kwa watu. Lakini pia anao uwezo wa kubadilisha sifa hiyo kwa kuhakikisha hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ugaidi ni zenye uwezo wa kuzaa matunda,” Mwisho wa kunukuu. Amesema kuwa, idara za usalama nchini Kenya zinalaumiwa kwa visa vya kutoweka kwa watu zaidi ya 34 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, eneo la Nairobi na Kaskazini Mashariki mwa nchi. Kwa mujibu wa Shirika la Muhuri, inaaminika kuwa, watu hao walikamatwa wakati wa oparesheni za kukabiliana na ugaidi maeneo yaliyotajwa. Naye Mkurugenzi Mkuu wa HRW Ken Roth amemtaka Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo kubuni tume ya uchunguzi ili watakaopatikana kuhusika na visa hivyo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. “Ikiwa Rais hatochukua hatua, basi tunatumai kwamba, bunge litachukua hatua. Huu ni mtihani kwa serikali kuthibitisha imejitolea kukomesha ukiukaji wa haki za kibinadamu,” alisema Roth. Shirika hilo limeongeza kuwa endapo tume itabuniwa basi inafaa kuwa tume huru itakayojumuisha pia wanachama ambao si watumishi wa serikali, na ripoti itolewe wazi kwa umma na ikabidhiwe kwa idara ya mahakama.