Uhusiano wa biashara ya mifugo baina ya Ethiopia na Djibouti waimarika baada ya kuzinduliwa reli
(last modified Tue, 24 Sep 2024 07:29:26 GMT )
Sep 24, 2024 07:29 UTC
  • Uhusiano wa biashara ya mifugo baina ya Ethiopia na Djibouti waimarika baada ya kuzinduliwa reli

Reli ya Ethiopia-Djibouti jana Jumatatu ilianza kusafirisha mifugo kutoka katikati mwa Ethiopia hadi bandarini nchini Djibouti ikiwa ni ishara ya kuzidi kuimarika uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili jirani za Pembe ya Afrika.

Takele Uma, afisa mkuu mtendaji wa Kampuni ya Ethio-Djibouti (EDR) amesema hayo katika taarifa yake na kupongeza kuwa, hatua hiyo itaboresha zaidi huduma za usafiri wa reli ya kilomita 752 kati ya nchi hizo mbili.

Amesema, huduma hiyo mpya ya usafirishaji wa mifugo itaimarisha kazi za reli ya EDR na kuboresha mauzo ya Ethiopia kwenye soko la kimataifa. Pia reli hiyo itatoa mchango mkubwa katika usafirishaji wa bidhaa zinazoingizwa Ethiopia kupitia Djbouti ambayo inapakana na Bahari Nyekundu.

Ethiopia ambayo ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na watu wengi baada ya Nigeria yenye takriban watu milioni 120, inajivunia kuwa na idadi kubwa ya mifugo barani Afrika, ikiwa na wastani wa ng'ombe milioni 70.3, kondoo na mbuzi milioni 95.4 na ngamia milioni 8.1. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za karibuni kabisa za Benki ya Dunia.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa reli hiyo ilikuwa imesafirisha abiria 680,000 na tani milioni 9.5 za mizigo kufikia Mei 2024, na wastani wa mapato ya kila mwaka ya ongezeko la asilimia 39 katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Tangu mwaka wa 2018, reli hiyo imeendeleza soko lake la mizigo na kupanua huduma zake, ikiwa ni pamoja na usafiri, treni za abiria kwa wanavijiji na treni maalum za usafiri wa magari.