Uchunguzi wa maoni: Sura ya Marekani imeporomoka duniani kote
(last modified Tue, 13 May 2025 07:03:05 GMT )
May 13, 2025 07:03 UTC
  • Uchunguzi wa maoni: Sura ya Marekani imeporomoka duniani kote

Utafiti mpya wa kila mwaka, uliochapishwa jana Jumatatu, unaonyesha kuwa mtazamo wa kimataifa kuhusu Marekani umerudi nyuma kwa kiasi kikubwa katika mwaka uliopita, na kwamba mtazamo wa watu kuhusu nchi hiyo sasa ni mbaya zaidi ikilinganishwa na Uchina.

Utafiti huo uliofanywa na Alliance of Democracies Foundation kwa ushirikiano na kampuni ya uchunguzi wa maoni ya Nera Data, umetokana na maoni ya washiriki zaidi ya 111,000 kutoka kote duniani na ulikusanywa kati ya Aprili 9 na 23.

Ingawa ripoti hiyo haikueleza kwa undani vigezo vilivyotumika katika tathmini hiyo, shirika lililosimamia uchunguzi huo linasisitiza kuwa lengo lake kuu ni kutetea na kukuza maadili ya kidemokrasia duniani kote.

Akielezea sababu ya mdororo huo mkubwa, Katibu Mkuu wa zamani wa NATO na mwanzilishi wa Alliance of Democracies Foundation, Anders Fogh Rasmussen, amesema sera zinazofuatwa na Rais wa Marekani, Donald Trump zimechangia kudidimiza sura ya nchi yake duniani kote.

"Rais Trump ameanzisha vita vya kibiashara, amemfokea hadharani rais wa Ukraini katika Ofisi ya Oval ndani ya White House na kuwafanya washirika wa Marekani wahisi hatari huku wapinzani wakipata ujasiri zaidi," ameongeza Fogh Rasmussen.

Malumbano ya Trump na Zelenskyy, White House

Matokeo haya yanaakisi kile ambacho waangalizi wamekielezea kuwa ni "kushuka kwa imani ya kimataifa kwa mtindo wa demokrasia ya Marekani," hasa kwa kuzingatia migawanyiko ya kisiasa ya ndani, shutuma za uingiliaji wa nchi za kigeni katika chaguzi na ukosoaji unaokua wa viwango vya haki za binadamu na haki za kijamii ndani ya Marekani yenyewe.