"Iran imeazimia kweli kufikia makubaliano katika mazungumzo ya nyuklia"
Rais wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko "jadi" katika mazungumzo yake yasiyo ya moja kwa moja na Marekani ili kufikia makubaliano yenye msingi wa amani, na kusisitiza azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuendelea kutekeleza shughuli zake za amani za nyuklia.
"Tunajadiliana [kwa dhati] kwa sababu tunataka amani," Masoud Pezeshkian alisema jana Jumapili, huku akisisitiza kwamba nchi hii haitaacha mafanikio yake ya nyuklia, hasa katika nyanja ya nishati ya amani.
"Tutaendelea kufuatilia shughuli hizi za amani kwa njia ya nguvu," ameongeza Dakta Pezeshkian, akihutubia mkutano wa baraza la mawaziri hapa Tehran jana Jumapili.
Hata hivyo, amepuuzilia mbali matakwa ya Marekani kuhusu miundombinu ya nyuklia ya Iran, na kuyataja kuwa "hayakubaliki," huku akisisitiza kwamba Iran "itaendelea kutekeleza shughuli hizo za amani kwa njia yenye nguvu."
Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu haiafiki takwa la kuvunjwa kwa miundombinu yake yote ya nyuklia ikisisitiza kuwa wazo hilo "halikubaliki."
Kwa miaka mingi sasa, Marekani na waitifaki wake wamekuwa wakiituhumu Jamhuri ya Kiislamu kwa kufuatilia “silaha za nyuklia,” licha ya matamko thabiti ya Iran kwamba haitafuti wala haihifadhi silaha hizo kwa mujibu wa kanuni zake za kimaadili na kidini.
Marekani na waitifaki wake wametumia madai hayo kuilenga Jamhuri ya Kiislamu kwa vikwazo vingi haramu na vya upande mmoja.
Duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani ilifanyika jana Jumapili, Mei 11, 2025, Muscat, mji mkuu wa Oman, kwa muda wa saa tatu.
Baada ya kumalizika mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: "Mazungumzo hayo yalikuwa mazito zaidi, yenye umakini zaidi, yaliyo wazi zaidi na yanayoangalia mbele zaidi kuliko duru tatu zilizopita."